JUMANNE JUMA 3 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.10:1-10
Kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile
wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao. Kama ndivyo, je! Dhabihu
hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na
dhambi? Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka. Maana haiwezekani damu ya
mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini
mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema,
Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo,
Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo
(zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako.
Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa
mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.40:1,3,6-7,10 (K)7,8
1. Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu.
Akatia wimbo mpya kinywani mwangu,
Ndio sifa zake Mungu wetu.
(K) Tazama nimekuja, kuyafanya mapenzi yako, Ee Bwana.
2. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)
3. Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa. (K)
SHANGILIO: Yak.1.21
Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole lile neno lililopandwa mioyoni mwenu,
ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu.
Aleluya.
INJILI: Mk.3:31-35
Walikuja mamaye na nduguze; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa wameketi,
wakimzunguka, wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta. Akawajibu, akisema,
Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani? Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema,
Tazama, mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana mtu ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye
ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu unayesifiwa na kutukuzwa hata na malaika
tunakutolea dua zetu kwa ajili ya Taifa lako tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Baba Baba Mtakatifu wetu F. afya na
nguvu ya kuendelea kulichunga kundi
ulilomkabidhi hapa duniani. Ee Bwana.
2. Dhabihu na sadaka zinazotolewa na makuhani wako
kwa ajili ya Taifa zima, daima zifikishwe mbele
ya kiti chako cha enzi na malaika wako watakatifu.
Ee Bwana.
3. Watawala wa dunia wajaliwe kuheshimu uhuru wa
dini na wa maabudu yasiyopingana nawe. Ee Bwana.
4. Kila mmoja wetu atambue kuwa udugu na upendo wa
kweli upo katika kutimiza mapenzi yako. Ee Bwana.
5. Malaika wako wawapeleke ndugu zetu marehemu
kwenye ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.