JUMANNE JUMA 4 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.12:1-4
Kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito,
na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa
mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya
furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume
wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna
hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita
hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi;
WIMBO WA KATIKATI: Zab.22:25-27,29-31 (K)26
1. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao.
Wapole watakula na kushiba,
Wamtafutao Bwana watamsifu;
Mioyo yenu na iishi milele.
(K) Wanaokutafuta, Ee Bwana, watakusifu.
2. Miisho yote ya dunia itakumbuka,
Na watu watamrejea Bwana;
Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu,
Humwinamia wote washukao mavumbini;
Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake, (K)
3. Wazao wake watamtumikia.
Zitasimuliwa habari za Bwana,
Kwa kizazi kitakachokuja,
Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake,
Ya kwamba ndiye aliyeyafanya. (K)
SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli,
Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.
INJILI: Mk.5:21–43
Yesu alipokwisha kuvuka kurudia ng’ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu;
naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo;
hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika
kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye.
Mkutano mkuu wakamfuata, wakimsongasonga. Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka
kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyonavyo,
kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya; aliposikia habari za Yesu,
alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana, alisema, Nikiyagusa mavazi yake
tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba
amepona msiba ule. Mara yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka
kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je!
Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote
ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka,
akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, Imani yako
imekuponya, enenda zako kwa Amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Hata alipokuwa katika
kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa;
kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu
wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na
Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu
wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia
na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote,
akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo
yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia,
Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili.
Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, tumwombe Mungu anayeheshimiwa na
kutukuzwa hata na malaika, tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwaimarishe viongozi wote wa Kanisa katika
kumwakilisha vema Kristo Mwanao, mwenye
kuianzisha na kuitimiza imani yetu. Ee Bwana.
2. Watawala wote duniani wajihusishe kwa karibu zaidi
kuiweka kando mizigo yote inayowakabili raia wao.
Ee Bwana.
3. Kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yao,wakristo
wote wawe tayari kuyastahimili mateso na adha
zote, kwa sababu ya imani yao kwako. Ee Bwana.
4. Ufute machozi ya wote wanaokulilia sababu ya vifo
vya wapendwa wao, sababu ya magonjwa au
matatizo mbalimbali ya maisha. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wafikishwe mbele ya kiti chako cha
enzi na kuuona uso wako mtukufu. Ee Bwana.
Ee Mungu unayewatuma malaika wako watukinge na
kila hatari, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.