JUMANNE JUMA 5 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.1:20–2:4
Mungu alisema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi
katika anga la mbingu. Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo
maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya
kuwa ni vyema. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na
wazidi katika nchi. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano. Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai
kwa jinsi zake, mnyama wa kufungwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo.
Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufungwa kwa jinsi zake, na kila kitu
kitaambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Na tufanye
mtu kwa mfano wetu; kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama,
na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake,
kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia,
Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani,
na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu,
ulio juu ya uso wan chi yote, pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula
chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho
juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila
kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita. Basi mbingu na
nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya;
akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba,
akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba
na kuifanya. Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.8:3–8 (K)1
1. Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako,
Mwezi na nyota ulizoziratibisha;
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie?
(K) Wewe Mungu, Bwana wetu,
jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote.
2. Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi ya mikono yako;
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. (K)
3. Kondoo, na ng’ombe wote pia;
Naam, na wanyama wa kondeni;
Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitiacho njia za baharini. (K)
SHANGILIO: Zab.27:11
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unifundishe njia yako,
na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya.
INJILI: Mk.7:1-13
Mafarisayo, na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele yake, wakaona
wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. Kwa maana
Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee
wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika,
kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba. Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza,
Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi?
Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu
kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo
ya wanadamu, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema!
Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu. Maana Musa alisema, Waheshimu baba yako na
mama yako, na, Amtukanaye babaye au mamaye kufa na afe. Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye
au mamaye, Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu cho chote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi;
wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye au mamaye; huku mkilitangua neno la Mungu kwa
mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa imani na matumaini tumwelekezee maombi
yetu Mungu mwumbaji, Mtawala na mmiliki wa vyote,
tukisema:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Viongozi wote wa Kanisa waimarike katika kulichunga
kundi la waamini wako, kwa kufundisha
neno lako, kutoa masakramenti na huduma
mbalimbali. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka wajue kwamba ingawa wanadamu
walipewa cheo cha ufalme wa ulimwengu
wote, wanayo dhamana ya kuongoza badala yako na
kama utakavyo Wewe. Ee Bwana.
3. Uyajalie mataifa yote kutambua kuwa hakuna
Mungu kama Wewe; ushikaye maagano na rehema
kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa
mioyo yao yote. Ee Bwana.
4. Uamshe ndani ya vijana wenye wito wa ndoa,
ari ya kubariki ndoa zao, kadiri ya sheria yako ya
tangu mwanzo wa maisha hayo. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapokelewe na malaika wako na
kupewa uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, Wewe wayaridhia mapokeo yasiyopingana
nawe. Uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu. Amina.