JUMANNE JUMA 6 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.6:5–8,7:1–5,10
Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analoliwaza moyoni
mwake ni baya tu sikuzote. Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.
Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na
kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema
machoni pa Bwana. Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana
nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki. Katika wanyama wote walio safi ujitwalie
saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke. Tena katika ndege
wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote. Kwa maana baada
ya siku saba nitainyesha dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya
juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali. Nuhu akafanya kama vile Bwana alivyomwamuru. Ikawa baada ya
siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.29:1–4,9–10 (K)11
1. Sauti ya Bwana, enyi wana wa Mungu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa Amani.
2. Sauti ya Bwana I juu ya maji,
Bwana yu juu ya maji mengi
Sauti ya Bwana ina nguvu,
Sauti ya Bwana ina adhama. (K)
3. Sauti ya Bwana yawazalisha ayala,
Na ndani ya hekalu lake wanasema wote, Utukufu.
Bwana aliketi juu ya Gharika;
Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele. (K)
SHANGILIO: Zab 25:4,5
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unijulishe njia zako,
unifundishe mapito yako.
Aleluya.
INJILI: Mk.8:14–21
Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza,
akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Wakabishana wao kwa
wao, kwa kuwa hawana mikate. Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna
mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio,
hamsikii? Wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu
vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua
makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba. Akawaambia, Hamjafahamu bado?
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, katika malaika tuutukuze wema na utukufu
wa Mungu, hasa tunaposali:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Malaika wako wawalinde Baba Mtakatifu na viongozi
wote wa dini dhidi ya maovu, ili waamini wapate
ari ya kutenda mema. Ee Bwana.
2. Ulikinge taifa letu na majanga yanayoleta uharibifu
wa mali na maisha ya watu wako. Ee Bwana.
3. Usituache tuvutwe na kudanganywa na tamaa
mbaya ili, tukisha kuyastahimili majaribu, tuipokee
taji ya uzima uliyowaahidia wakupendao. Ee Bwana.
4. Kila mmoja wetu afuate maongozi ya malaika na kujiepusha
na dhambi, ili upendo wako utawala duniani kote. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wakusanywe kwako na kurithishwa
uzima wa milele. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwako, Ee Mungu, kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.