JUMANNE JUMA 7 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO: Ybs.2:1-11
Mwanangu, ukija kumtumikia Bwana, weka tayari roho yako kwa kujaribiwa. Ujitengeneze moyo ustahimili, wala usitaharuki siku ya kuteswa. Uambatane naye wala usijitenge tena, ili mwisho wako ukuzwe. Kila utakalopelekewa ulipokee kwa kuchangamka moyo, uyavumilie mabadiliko ya unyonge wako. Maana dhahabu ujaribiwa motoni, na wateule karibuni mwa unyonge. Basi umwamini yeye, naye atakusaidia; ukazinyoshe njia zako na kulikaza taraja lako katika yeye. Enyi mnaomcha Bwana, zingojeeni rehema zake, msigeuke upande msije mkaanguka. Enyi mnaomcha Bwana, mwaminini yeye sana, Thawabu yenu haitawapotea. Enyi mnaomcha Bwana sasa tarajieni mema, na furaha ya daima na rehema. Angalieni vizazi vya kale mkaone; nani aliyemtumaini Bwana akaaibika? Nani aliyekaa hali ya kumcha akaachwa? Nani aliyemwita akadharauliwa? Mradi Bwana yu mwenye huruma na rehema, husamehe dhambi na kuokoa wakati wa shida.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.37:3-4,18-19,27-28,39-40 (K)5
1. Umtumaini BWANA ukatende mema,
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa BWANA,
Naye atakupa haja za moyo wako.

(K) Umkabidhi BWANA njia yako,
Pia umtumaini, naye atafanya.

2. BWANA anazijua siku za wakamilifu,
Na urithi wao utakuwa wa milele.
Hawataaibika wakati wa ubaya,
Na siku za njaa watashiba. (K)

3. Na kukaa hata milele.
Kwa kuwa BWANA hupenda haki,
Wala hawaachi watauwa wake.
Wao hulindwa milele,
Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa. (K)

4. Na wokovu wa wenye haki una BWANA;
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye BWANA huwasaidia na kuwaopoa;
Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa;
Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)

SHANGILIO: Gal.6:14
Aleluya, aleluya,
Mbali na mimi kuwa na utukufu
isipokuwa msalabani wa Bwana wetu Yesu Kristo,
ambalo dunia imesulubiwa kwangu,
na mimi ulimwenguni.
Aleluya.

INJILI: Mk.9:30–37
Yesu na wanafunzi wake wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yu aenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza. Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa. Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, tukimwamini Mungu, Yeye atatusaidia: Basi, kwa imani tuombe.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie wakubwa wote wa Kanisa kujitoa daima kwa ajili ya kuwatumikia watu wako. Ee Bwana.

2. Wote wenye mamlaka hapa duniani wajaliwe imani, uchaji na unyenyekevu kwako, wapate kuwafikisha watu wako kwenye lengo halisi la maisha. Ee Bwana.

3. Kwa msaada wa malaika wako watakatifu, tujaliwe kuyastahimili majaribu, wala tusitaharuki siku ya kuteswa. Ee Bwana.

4. Utujalie utii kwako, tumpinge shetani, tukukaribie kwa utakaso na usafi wa moyo; tupate kuwa marafiki wako. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wakijongee kiti cha rehema yako na kupewa wokovu wa milele. Ee Bwana.

Ee Mungu, Mwanao amesema: anayempokea Yeye akupokea Wewe uliyemtuma. Uyapokee maombi yetu kwa jina la huyo Kristo Bwana wetu. Amina.