JUMANNE JUMA 8 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO: YbS.35:1-12
Mwenye kuishika torati ndiye azidishaye matoleo; mwenye kuziangalia amri ndiye aitoaye kafara ya amani; amlipaye mwenzake hisani yake hutoa sadaka ya unga bora; naye atoaye sadaka kwake maskini hutoa dhabihu ya kushukuru. Kuuacha uovu kwampendeza Bwana, na kujitenga na udhalimu ni kipatanisho. Lakini ujihadhari usitokee mbele za Bwana mikono mitupu; maana sharti hayo yote yatendeke kwa ajili ya amri. Toleo lake mwenye haki lina kibali madhabahuni, na harufu tamu yake yafika mbele zake Aliye juu. Dhabihu ya mwenye haki yakubalikana, wala kumbukumbu lake halisahauliki. Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili. Kwa kila kitolewacho uoneshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko. Mpe Mungu kama alivyokupa wewe; na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu. Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa ni yeye; kwa kuwa Bwana hulipa, naye atakulipa wewe mara saba. Usidhanie kuwa unaweza kutoa rushwa, kwa maana Yeye hazipokei; wala usiwaze moyoni kutoa dhabihu ya jeuri, kwa kuwa Bwana ndiya mhukumu wala hakijali cheo cha mtu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.50:5-8,14,23 (K)23
1. Nikusanyieni wacha Mungu wangu
Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
Na mbingu zitatangaza haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.

(K) Nitamwonesha wokovu wa Mungu
autengenezaye mwenendo wake.

2. Sikieni, enyi watu wangu, nami nitanena,
Mimi nitakushuhudia, Israeli;
Mimi ndimi niliye Mungu, Mungu wako.
Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele zangu daima. (K)

3. Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru,
Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
Atoaye dhabihu za kushukuru,
Ndiye anayenitukuza.
Naye autengenezaye mwenendo wake,
Nitamwonesha wokovu wa Mungu. (K)

SHANGILIO: Lk.8:15
Aleluya, aleluya!
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao
hulisikia neno la Mungu.
Aleluya!

INJILI: Mk.10:28-31
Petro alimwambia Yesu, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe. Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, ingawa malaika wanastahili kuheshimiwa sana, Wewe wajidhihirisha kuwa Mkuu na mwenye kustahili heshima kupita vitu vyote. Na hivi twakuomba.

Kiitikio: Utupe neema yako.
1. Upende kuwaimarisha Maaskofu na Mapadre wetu katika kukutolea dhabihu safi na yenye harufu nzuri madhabahuni pako Wewe uliye juu. Ee Bwana.

2. Wanaotoa au kupokea rushwa wajaliwe neema ya kuacha kabisa dhambi hiyo, wakijua kwamba Wewe Mungu hupokei rushwa wala dhabihu ya jeuri, na kwamba hujali cheo cha mtu. Ee Bwana.

3. Utujalie moyo wa kuwasaidia maskini na wasiojiweza, na kulihudumia Kanisa lako kwa moyo mkunjufu. Ee Bwana.

4. Utudumishe katika kuyaishi mambo tuliyofunuliwa katika Maandiko matakatifu, na ambayo Malaika wanatamani kuyachungulia; tupate kuwa watakatifu kama Wewe. Ee Bwana.

5. Ndugu zetu marehemu wapate kibali cha kuingia katika ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayesifiwa hata na malaika, upokee sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.