JUMATANO JUMA 1 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1:Ebr.2:14-18
Kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti
amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa
hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao
wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema,
mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa
alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:1-4,6-9 (K)8
1. Mshukuruni Bwana, liitieni jina,
Wajulisheni watu matendo yake.
Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.
2. Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake siku zote. (K)
3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)
4. Analikumbuka agano lake milele;
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
Agano alilofanya na Ibrahimu,
Na uapo wake kwa Isaka. (K)
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya!
INJILI: Mk.1:29-39
Siku ile, Yesu alipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na
Yakobo na Yohane. Naye mkewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara
wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia.
Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi,
na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi
mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. Hata alfajiri
na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. Simoni
na wenziwe wakamfuata; nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. Akawaambia, Twendeni
mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea.
Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Bwana Mungu, Mwanao Yesu Kristo alipaswa
kufananishwa na sisi ndugu zake katika mambo yote,
isipokuwa kwa habari ya dhambi, ili afanye suluhu kwa
dhambi zetu. Basi tunakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na Maaskofu wetu wote
wazidishiwe neema za ukuhani wa Mwanao Yesu
Kristo. Ee Bwana.
2. Wote wenye dhamana ya kuwaongoza raia wenzao
wazuie utumwa wa aina yoyote. Ee Bwana.
3. Uwajalie vijana wetu kuitikia miito mitakatifu na
uamshe ndani yao moyo wa kuwajali na kuwatii
wakubwa, walimu na walezi wao. Ee Bwana.
4. Umjalie kila mmoja wetu kuuishi kiaminifu wito
uliomjalia. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapate rehema yako na kushirikishwa
ufufuko wa Mwanao. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetujalia moyo wa sala na roho ya kimisionari,
uisikie sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.