JUMATANO JUMA 24 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 1Kor.12:31-13:13
Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonesha njia iliyo bora. Nijaposema kwa lugha
za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena
nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi
cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote
kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii
kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi
kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu,
bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.
Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma,
yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa
sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga,
nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga;
tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona
kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu;
wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini,
upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:2-5,12,22(K)12
1. Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
Mwimbieni wimbo mpya,
Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.
2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminfu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)
3. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe. (K)
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya!
INJILI: Lk.7:31-35
Yesu aliwaambia makutano: Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao wamefanana na nini?
Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza;
tuliomboleza, wala hamkulia. Kwa kuwa Yohane Mbatizaji alikuja, hali mkate wala hanywi divai,
nanyi mwasema, ana pepo. Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema, Tazama,
mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi. Na hekima imejulikana
huwa ina haki kwa watoto wake wote.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kanisa ni nyumba ya Mungu na mahali rasmi
pa kukutana na kuongea naye. Kwa vile yupo tayari
kutusikiliza, tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie wachungaji wetu udumifu katika kuwaelekeza
kwa upole watu wote, kuitikia mwito wa kulitunza na
kulitumia vema kanisa lako. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za viongozi wa serikali, asasi na
taasisi zake, katika kutimiza amri yako ya upendo
kwa watu wote. Ee Bwana.
3. Wote waliojitenga nawe na wenye dhambi wajaliwe
moyo wa kumkaribia Mwanao, Yesu Kristo, aliyekuja
kwa ajili yao. Ee Bwana.
4. Sisi sote tujaliwe kuijua siri kuu ya utaua, tupate
kukudhihirisha na kukuhubiri kwa mataifa, ili nao
wapate kukuamini na kuokoka. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapokelewe huko mbinguni na kupewa
uzima wa milele. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetaka hekima ijulikane kuwa ina haki kwa
watoto wake wote, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.