JUMATANO JUMA 25 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Mit.30:5-9
Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio. Usiongeze neno katika maneno
yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo. Mambo haya mawili nimekuomba; Usininyime kabla
sijafa. Usiondolee ubatili na uongo; Usinipe umaskini wala utajiri; unilishe chakula kilicho
kadiri yangu. Nisije nikashiba nikakukana, Nikasema, Bwana ni nani? Wala nisiwe maskini sana
nikaiba, Na kulitaja bure jina la Mungu wangu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:29,72,89,101,104,163(K)105
1. Uniondolee njia ya uongo,
Unineemeshe kwa sheria yako.
Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
(K) Neno lako ni taa ya miguu yangu.
2. Ee Bwana, neno lako lasimama,
Imara mbinguni hata milele.
Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya,
Ili nilitii neno lako. (K)
3. Kwa mausia yako najipatia ufahamu,
Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.
Nimeuchukia uongo, umenikirihi,
Sheria yako nimeipenda. (K)
SHANGILIO: 1Sam.3:9
Aleluya, aleluya!
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia, wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya!
INJILI: Lk.9:1-6
Yesu aliwaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi.
Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa. Akawaambia, Msichukue kitu kwa safari
yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili. Na nyumba
yoyote mtakayoingia kaeni humo, mpaka mtoke humo. Na wale wasiowakaribisha, mtokapo katika mji huo,
yakung’uteni hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa ushuhuda juu yao. Wakaenda, wakazunguka katika
vijiji, wakihubiri Injili na kupoza watu kila mahali.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu amemwita kila mmoja wetu kama
alivyo, ili akaitangaze Injili yake. Kwa vile ni wajibu
mkubwa, nasi tu dhaifu, tuombe neema yake.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Askofu wetu F. na Mapadre wetu wote
afya na nguvu, wapate kutekeleza sawa sawa kazi za
kitume, ulizowakabidhi kwa ajili ya Kanisa lako.
Ee Bwana.
2. Wote waliodhaminiwa kuwatawala watu badala yako
wajaliwe kuwatumikia watu wako kadiri ya mapenzi
yako. Ee Bwana.
3. Umwepushe na maovu kila mmoja wetu, ili
tuondokane na utumwa wa dhambi, na kuwa mfano
mzuri wa fadhila kwa wenzetu. Ee Bwana.
4. Utuondolee ubatili na uwongo; utukarimu kadiri ya
kipimo tunachohitaji; na utujalie kutolitaja bure
Jina lako Takatifu. Ee Bwana.
5. Uwakumbuke ndugu zetu marehemu na uwashirikishe
uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunayaleta maombi yetu haya kwako, Ee Mungu Baba,
kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.