JUMATANO JUMA 27 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Gal.2:12,7-14
Baada ya miaka kumi na mine, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na
Tito pamoja nami. Nami nalikwenda kwa kuwa nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika
Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio
bure. Bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile
Petro ya waliotahiriwa. Maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha
mimi kwenda kwa mataifa. Tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohane,
wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa
mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara; ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami
neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya. Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso
kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu. Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kwa
Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga,
huku akiwaogopa waliotahiriwa. Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata Barnaba pia
akachukuliwa na unafiki wao. Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya
Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za mataifa, wala
si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha mataifa kufuata desturi za Wayahudi?
WIMBO WA KATIKATI: Zab.117(K)Mk.16:15
Aleluya.
1. Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini.
(K) Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
2. Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)
SHANGILIO: Yak.1:18
Aleluya, aleluya!
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli,
tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya!
INJILI: Lk.11:1-4
Yesu alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia,
Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake. Akawaambia,
Msalipo, semeni: Baba, Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, Utupe siku kwa siku riziki yetu.
Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu ni mwenye neema, amejaa huruma, si
mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema; naye hughairi
mabaya. Tumwombe:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Wachungaji na wahubiri wote wa neno lako wafurahie
kazi yao waonapo wakosefu wanatubu na kukuongokea Wewe. Ee Bwana.
2. Ufalme wako uje katika ulimwengu huu uliojaa
maovu, ili watu wako waondokane na ubinafsi na
mambo yote ya anasa za dunia. Ee Bwana.
3. Umjalie kila mmoja wetu moyo wa sala katika
mazingira yoyote: katika majaribu, katika mashaka,
katika taabu na hata katika raha. Ee Bwana.
4. Utuepushe na woga au unafiki katika utume wetu,
ili ukweli wa neno lako upate kuhubiriwa bila
ubaguzi kwa watu wote na katika mazingira yoyote. Ee Bwana.
5. Kwa huruma yako, marehemu wetu waione nuru
ya uso wako mtukufu huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayefurahi kuona wakosefu wanatubu na
kukurudia Wewe, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.