JUMATANO JUMA 29 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Efe.3:2-12
Mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa
nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache. Kwa hayo, myasomapo,
mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika
vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya
kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi
wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake,
kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake. Mimi, niliye
mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri
wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu
zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya
Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya
kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa
kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.
WIMBO WA KATIKATI: Isa.12:2-6(K)3
1. Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu
Na wimbo wangu;
Naye amekuwa wokovu wangu.
Basi, kwa furaha mtateka maji
Katika visima vya wokovu.
(K) Kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu.
2. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
Litajeni jina lake kuwa limetukuka.
Mwimbieni Bwana. (K)
3. Kwa kuwa ametenda makuu,
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)
SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Mtu akinipenda, atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda, na sisi tutakuja kwake.
Aleluya!
INJILI: Lk.12:39-48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja
mwivi; angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa
msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu. Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu,
au watu wote pia? Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana
wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye
bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini,
mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume
kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua,
atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini. Na mtumwa yule aliyejua mapenzi
ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye
amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi;
naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa kuwa saa tusiyodhani ndiyo ajayo
Mwana wa Adamu, tusali kwa Mungu tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Upokee shukrani zetu kwa kuwa umewaweka
Maaskofu kuwa mawakili wako wenye busara, wapate
kuwa juu ya utumishi wa Kanisa lako na kuwaandaa
watu kwa ujio wa Mwanao. Ee Bwana.
2. Viongozi wetu wa serikali waimarishe mahusiano
mazuri na Mataifa jirani, kwani ni warithi pamoja
nasi wa urithi mmoja, na washiriki pamoja nasi wa
ahadi yako ya ukombozi. Ee Bwana.
3. Uwaongoe watumwa wa dhambi, wapate kuungojea
ujio wa Bwana kwa saburi. Ee Bwana.
4. Umjalie kila mmoja wetu kuwa mtumwa wa haki, kwa
kukesha kila siku na kuzitii amri zako. Ee Bwana.
5. Wote waliomaliza safari yao hapa duniani wapewe
rehema yako na uzima usio na mwisho huko kwenye
makao yako ya milele. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyesema kila aliyepewa vingi atatakiwa kutoa
vingi vile vile, uyapokee maombi haya tuliyokutolea.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.