JUMATANO JUMA 2 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Isa.40:25-31
Mtanifananisha na nani, nipate kuwa sasa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu. Inueni macho yenu juu,
mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu
wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake. Mbona
unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu
imempita Mungu wangu asiiangalie? Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba
miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea
nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Haya vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao
wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka;
watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.103:1-4,8,10
1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Naam, vyote vilivyo ndani yangu,
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote. (K)
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
2. Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)
3. Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Hakututenda sawasawa na hatia zetu.
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Tazama Bwana atakuja kuwaokoa watu wake, Heri walio tayari kumlaki.
Aleluya.
INJILI: Mt.11:28-30
Siku ile, Yesu alijibu akasema: Njoni kwangu nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini
mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa katika Kristo, kwa kuwa sisi ni watu dhaifu, na Bwana Mwenyezi huwapa nguvu waliochoka, tumwombe
atuimarishe:
Kiitikio: Twaomba huruma yako.
1. Wewe uliye peke yako Mtakatifu, kwa Kipindi hiki cha Majilio, umwongezee Askofu wetu F. ari
ya kulichunga kundi lako kiaminifu, ili kundi hilo lifanane zaidi nawe. Ee Bwana.
2. Uyaelekeze macho yetu huko juu, ili tukuone wewe muumba wetu na kukupokea wakati wake. Ee Bwana.
3. Uzibue masikio yetu, ili yasikie sauti yako; na akili zetu ziyatambue makusudio yako. Ee Bwana.
4. Uwaite kwako wote wasumbukao na wanaolemewa na mizigo ya dhambi, ili wajifunze kwako na, wakiisha tubu,
waishi katika amani yako. Ee Bwana.
Ee Mungu, Mwanao ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; na anatualika sote twende kwake tukapate raha nafsini
mwetu. Utuondolee mizigo inayotukwaza, ili tuwe wepesi kukujia wewe. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.