JUMATANO JUMA 2 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.7:1-3,15-17
Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa
akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu
vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme
wa amani; hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake,
bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele. Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana
zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki; asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri
iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo; maana ameshuhudiwa kwamba, Wewe u
kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.110:1-4 (K)4
1. Neno la Bwana kwa Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume,
Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.
(K) Ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.
2. Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako.
Uwe na enzi kati ya adui zako; (K)
3. Watu wako wanajitoa kwa hiari,
Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu,
Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako. (K)
4. Bwana ameapa, Wala hataghairi,
Ndiwe kuhani hata milele,
Kwa mfano wa Melkizedeki. (K)
SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya!
INJILI: Mk.3:1-6
Yesu aliingia katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza; wakamvizia ili
kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki. Akamwambia yule mtu mwenye mkono
uliopooza, Simama katikati. Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda
mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza. Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona
huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha;
mkono wake ukawa mzima tena. Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake
pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tunahitaji sana msaada wa Mungu, ili
kutenda mema daima katika ulimwengu huu. Basi na
tumwombe Mungu tukisema:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Viongozi wa Kanisa wadumu katika kuuishi
ukuhani, kwa kutoa vipawa na dhabihu safi mbele
yako, kwa ajili ya wokovu wao wenyewe na wa
watu wako. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia waheshimu uhuru wa dini, ili
watu wako wapate huduma wanazostahili kimwili na
kiroho. Ee Bwana.
3. Utujalie imani, matumaini na moyo mkuu dhidi ya
maadui wetu katika kutimiza mapenzi yako. Ee
Bwana.
4. Kwa maombezi ya Mtakatifu Yosefu, tujaliwe kuishi
kitakatifu siku zote, tukisaidiana katika taabu na raha.
Ee Bwana.
5. Wagonjwa wetu wapone na marehemu wote
wapokelewe kwako mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.