JUMATANO JUMA 30 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Efe.6:1-9
Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia. Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana. Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo; wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekezao kwa wanadamu; bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo; kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu; mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana, kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru. Nanyi, akina bwana, watendeeni wao yayo hayo, mkiacha kuwaogofya, huku mkijua ya kuwa yeye aliye Bwana wao na wenu yuko mbinguni, wala kwake hakuna upendeleo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:10-14(K)10
1. Ee Bwana kazi zako zote zitakushukuru,
Wacha Mungu wako watakuhimidi,
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.
Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.

(K) Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru.

2. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)

3. Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini. (K)

SHANGILIO: 1Sam.3:9;Yn.6:68
Aleluya, aleluya!
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia, wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya!

INJILI: Lk.13:22-30
Yesu alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akamwambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia wasiweze, wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.