JUMATANO JUMA 31 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Flp.2:12-18
Wapendwa wangu, kama vile mlivyotii siku zote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu, mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya Kristo, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure. Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote. Nanyi vivyo hivyo furahini, tena furahini pamoja nami.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.27:1,4,13-14(K)1
1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?

(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

2. Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)

3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

SHANGILIO: Lk.8:15
Aleluya, aleluya!
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya!

INJILI: Lk.14:25-33
Makutano mengi walipokuwa wakifuatana na Yesu, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za Amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhlika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu,Wewe ni upendo na umetuhimiza kupendana, kwa kuwa pendo ndilo utimilifu wa sheria. Basi, twakuomba:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na Maaskofu wote wazidi kulipenda Kanisa ulilowakabidhi, lipate kustawi kimwili na kiroho siku hadi siku. Ee Bwana.

2. Viongozi wenye dhamana ya kuwahudumia watu, serikalini na kwenye taasisi na sekta binafsi, watende mambo yote pasipo manung'uniko wala lawama yoyote. Ee Bwana.

3. Wote wasiolitukuza jina lako wajaliwe kujihoji na kujipatanisha nawe kwa upendo kabla ya siku ya hukumu. Ee Bwana.

4. Msalaba wa Kristo utukumbushe daima juu ya sadaka tunayopaswa kukutolea Wewe Mungu, kwa kuacha yote na kukufuata kwa upendo. Ee Bwana.

5. Ndugu zetu marehemu waliojitahidi kuuishi upendo wapewe huruma yako na kuurithi ufalme wako wa mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka tuyafanye yote kwa upendo, uyapokee maombi yetu.Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.