JUMATANO JUMA 32 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Tit.3:1-7
Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila
kazi njema; wasimtukane mtu yeyote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionesha upole wote kwa watu
wote. Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku
tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na
kuchukiana. Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa,
ulituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa
kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia
ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa
uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.23(K)1
1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Huniuisha nafsi yangu.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu.
2. Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake,
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya,
Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
3. Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)
4. Hakika wema na fadhili zitanifuata,
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
SHANGILIO: Zab.19:11-19
Aleluya, aleluya!
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya!
INJILI: Lk.17:11-19
Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, Yesu alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya.
Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza
sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajioneshe kwa
makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi,
huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa
Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! Hawakuonekana
waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, Imani yako imekuokoa.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu anatualika kujifunza hekima, kumjali,
kumtegemea yeye katika taabu na raha, na kumshukuru
kwa mema anayotujalia. Kwa imani, tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie Maaskofu wetu na Wachungaji wote wa
Kanisa lako ari mpya ya kitume, wapate
kuwahudumia vema zaidi waamini wao kimwili na
kiroho. Ee Bwana.
2. Wafalme wa dunia wajaliwe kukumbuka kuwa
walipewa falme na milki zao nawe Bwana uliye
juu, na uwawezeshe kutimiza wajibu zao kwa
hekima. Ee Bwana.
3. Sisi sote tujaliwe kutoa hukumu kwa adili, kuzishika
sheria, kufuata mafundisho yako na kukushukuru kwa
fadhili zako. Ee Bwana.
4. Tunawaombea hasa watoto, vijana na wanafunzi
wote, ili wawe na tabia njema; wakinyenyekea na
kutii kwa wenye mamlaka, na kuwa tayari kwa kila
kazi njema. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wahurumiwe dhambi zao na kustahilishwa
uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu usiye na upendeleo, uyapokee maombi yetu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.