JUMATANO JUMA 34 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Ufu.15:1-4
Mimi, Yohane, niliona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia. Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, wa wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kandokando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu. Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwanakondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-3,7-9(K)Ufu.15:3
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.

(K) Matendo yako ni makuu, Ee Bwana Mungu Mwenyezi.

2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machozi pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
Mito na ipige makofi,
Milima na iimbe pamoja kwa furaha. (K)

4. Mbele za Bwana;
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa adili. (K)

SHANGILIO: 1Thes.2:13
Aleluya, aleluya!
Lipokeeni neno la Mungu, siyo kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu.
Aleluya!

INJILI: Lk.21:12-19
Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwatia magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu. Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikirifikiri kwanza mtakavyojibu; Kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Wewe ndiwe unayetupatia msaada na nguvu. Kwa hiyo tunakuomba:-

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Baba Mtakatifu F., Maaskofu na Mapadre wazidi kuwaimarisha waamini wao katika imani, na kuwafunulia siri ya mateso ambayo yalimsibu hata Mwanao. Ee Bwana.

2. Wote wenye mamlaka wajaliwe hekima ya utawala bora, wapate kuwaongoza watu wao kwenye uhuru wa kweli, haki, amani na usawa. Ee Bwana.

3. Uwaepushe waamini wako na mambo ya uabudu sanamu au miungu; bali wakuabudu Wewe uliye pekee Mungu wa kweli na wa milele. Ee Bwana.

4. Tunakushukuru kwa matendo yako makuu na ya ajabu, kwa njia zako za haki na za kweli; na tunakuabudu na kulitukuza jina lako, kwa kuwa Wewe peke yako ni Mtakatifu. Ee Bwana.

5. Kwa huruma yako, marehemu wetu wasamehewe mapungufu yao, wapate kuurithi uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyesema kwamba kwa subira yetu tutaziponya nafsi zetu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.