JUMATANO JUMA 3 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Ebr.10:11-18
Kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema, Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.110:1-4 (K)4
1. Neno la Bwana kwa Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume,
Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.

(K) Wewe ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.

2. Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako.
Uwe na enzi kati ya adui zako; (K)

3. Watu wako wanajitoa kwa hiari, Siku ya uwezo wako;
Kwa uzuri wa utakatifu,
Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako. (K)

4. Bwana ameapa, Wala hataghairi,
Ndiwe kuhani hata milele,
Kwa mfano wa Melkizedeki. (K)

SHANGILIO: Yak.1.21
Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole lile neno lililopandwa mioyoni mwenu,
ambalo laweza kuziokoa nafsi zenu.
Aleluya.

INJILI: Mk.4:1-20
Yesu aliaanza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini, mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake, Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda; ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila. Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba; hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka. Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda. Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia. Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie. Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano. Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano, ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa. Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje? Mpanzi huyo hulipanda neno. Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao. Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa. Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai. Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, tukiongozwa na neno la Mungu lililopandwa mioyoni mwetu, tuombe msaada wa Mungu tukisema:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umlinde Baba Mtakatifu wetu F. na Kanisa lako lote. Ee Bwana.

2. Uwe pamoja na viongozi wetu wa Kanisa na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; tupate kufaidi malisho bora katika nyumba yako. Ee Bwana.

3. Uliepushe taifa letu na maadui wa ndani na nje; na wasuluhishi wa migogoro mbalimbali wafuate kanuni na sheria ziletazo haki, amani na usawa. Ee Bwana.

4. Sheria zako zitiwe mioyoni mwa watu wako, ili wasianguke katika dhambi wala uasi wowote, bali wazae matunda ya kudumu. Ee Bwana.

5. Uwatulize wagonjwa, uwafariji wafungwa na uwapokee huko mbinguni ndugu zetu marehemu. Ee Bwana.

Ee Mungu uliye nguvu na tegemeo la wote wakutumainio, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.