JUMATANO JUMA 4 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Ebr.12;4–7,11–15
Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi. Tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, wala usizimie moyo ukikemewa naye; maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi aisyerudiwa na babaye? Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye Amani. Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe. Tafuteni kwa bidii kuwa na Amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia kana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.103:1–2,13–14,17–18 (K)17
1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.

(K) Fadhili za Bwana zina wamchao
tangu milele hata milele.

2. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana awahurumia wamchao. Kwa maana yeye anatujua umbo letu Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi. (K)

3. Fadhili za Bwana zina wamchao Tangu milele na milele, Na haki yake ina wana wa wana; Wale washikao agano lake. (K)

SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana,
yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe,
bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya!

INJILI: Mk.6:1-6
Yesu alitoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao, wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jaama zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wowote huko; isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.

--------------

--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa kuwa utakatifu ni sharti muhimu la kufika mbinguni, hatuna budi kuomba neema ya Mungu. Basi na tumwombe tukisema:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwalinde Baba Mtakatifu wetu F., Askofu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa lako. Ee Bwana.

2. Uwakemee viongozi wa dunia wasiotenda haki kwa raia wao. Ee Bwana.

3. Uwajalie raia wote utii kwa viongozi wao katika mambo yote yenye tija kwa taifa na jamii kwa ujumla. Ee Bwana.

4. Sisi sote utuongezee juhudi ya kutafuta utakatifu ili. tukuone Wewe. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu washirikishwe amani yako huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka udumifu katika kuyatimiza mapenzi yako bila kujali kikwazo chochote, uipokee sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.