JUMATANO JUMA 5 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.2:4–9,15–17
Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni
haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyesha nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi; ukungu
ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi. Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi,
Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Bwana Mungu
akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. Bwana Mungu
akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati
ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani
ya Edeni, ailime na kuitunza. Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani
waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda
ya mti huo utakufa hakika.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.104:1–2,27–30. (K)1
1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Umejivika heshima na adhama.
Umejivika nuru kama vazi;
Umezitandika mbingu kama pazia;
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
2. Hao wote wanakungoja Wewe,
Uwape chakula chao kwa wakati wake.
Wewe huwapa,
Wao wanakiokota;
Wewe waukunjua mkono wako,
Wao wanashiba mema; (K)
3. Wewe wauficha uso wako,
Wao wanafadhaika;
Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wan chi. (K)
SHANGILIO: Zab.19:8
Aleluya, aleluya!
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya!
INJILI: Mk.7:14–23
Yesu aliwaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho
nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo
unajisi yule mtu. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Hata alipoingia nyumbani,
ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi
hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia
unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema
hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana
ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya,
ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka
ndani, nayo yamtia mtu unajisi.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa vile tunahitaji msaada wa Mungu katika
kuyatimiza mapenzi yake, tumwombe Mungu mwenyewe
tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu na Mapadre
wajaliwe kuepukana na hila za yule mwovu, ili
neno lako lizidi kuenea popote duniani. Ee Bwana.
2. Viongozi wote wajaliwe kuzidumisha sheria na kanuni
zinazoilinda na kuiendeleza dunia na viumbe vyake
kadiri ya mapenzi yako. Ee Bwana.
3. Utusaidie sisi sote kukumbuka kuwa dunia hii ndiyo
bustani tuliyopewa nawe, ili tuilime na kuitunza.
Ee Bwana.
4. Utuamshie moyo wa kukupa talanta na sifa unazostahili,
kwani Wewe ndiwe mfalme wetu na mpaji
wa vyote. Ee Bwana.
5. Kwa huruma yako, ndugu zetu marehemu watakaswe
roho zao na kufikishwa huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, uliye chemchemi ya kila kilicho chema,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.