JUMATANO JUMA 6 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.8:6–13,20–22
Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; akamtoa kunguru nje,
naye hakurudi bali aliruka huko na huko mpaka maji yalipokauka nchini. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji
yamepunguka usoni pa nchi; bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia
Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza
mle safinani. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia
jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua
ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie
tena kamwe. Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka
juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. Nuhu
akamjengea Bwana madhabahu; akamtwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi,
akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema
moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu
ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. Muda
nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazini
na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.116:12–15,18–19 (K)17
1. Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu,
Na kulitangaza jina la Bwana.
(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru,
ee Bwana.
2. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake. (K)
3. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote,
Katika nyua za nyumba ya Bwana,
Ndani yako, ee Yerusalemu. (K)
SHANGILIO: Efe.1:19–27
Aleluya, aleluya!
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo
ayatie nuru macho ya mioyo yetu,
tujue tumaini la mwito wetu jinsi lilivyo.
Aleluya!
INJILI: Mk.8:22–26
Siku ile, Yesu na wanafunzi wake, wakafika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse. Akamshika
mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza,
Waona kitu? Akatazama juu, akisema, Naona watu kama miti, inakwenda. Ndipo akaweka tena mikono yake juu
ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi. Akampeleka nyumbani kwake akisema,
Hata kijijini usiingie.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, safina ya Nuhu ni mfano wa Kanisa linalosafiri
hapa duniani, tena katika mazingira hatarishi. Tuombe
msaada wa Mungu tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Kwa neema yako viongozi wetu wa Kanisa wazidi
kukemea maovu, ili dunia idumishe amani na
upendo wako. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia watambue kuwa hawana ruhusa
ya kujiwekea sheria zilizo kinyume na maadili,
yaliyokusudiwa kwa watu wote tangu mwanzo wa
ulimwengu. Ee Bwana.
3. Utuepushe sisi sote na anasa za kidunia kwani yanaenda
kinyume na mapenzi yako. Ee Bwana.
4. Utukumbushe daima kuwa dini iliyo safi, isiyo na
taka mbele zako ni kwenda kuwatazama yatima,
wajane na wote wenye shida katika dhiki yao na
kujilinda na dunia pasipo mawaa. Ee Bwana.
5. Uwakaribishe ndugu zetu marehemu kwenye nyumba
yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo, Ee Baba, kwa njia ya Mwanao mpenzi,
Yesu Kristo Bwana wetu. Amina.