JUMATATU JUMA 1 MAJILIO
MASOMO

SOMO 1: Isa. 2:1-5
Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu. Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani mwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; maana katika Sayuni itatoka sheria na neno la Bwana katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 122:1-4, 8, 9
1. Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu. (K)

(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.

2. Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K)

3. Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu
Niseme sasa, Amani ikae nawe.
Kwa ajili ya nyumba ya Bwana, Mungu wetu,
Nikutafutie mema. (K)

Shangilio: Zab.80:4
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, Mungu wa majeshi, hata lini? Utayaghadhibikia maombi ya watu wako?
Aleluya.

INJILI: Mt. 8:5-11
Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu, lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, yeyote katika Israeli. Nami nawaambieni, kwamba, wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi na wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni.

--------------

--------------
MAOMBI
Tunakushukuru, Ee Mungu, kwa kutupatia Kipindi hiki cha Majilio ili tuutafakari ujio wa Mwanao. Na hivi twakuomba:

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwaongezee Baba Mtakatifu wetu F., Askofu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa lako ari ya kutukumbusha daima juu ya ujio wa Mwanao. Ee Bwana.

2. Sheria za serikali zisipingane na Neno lako, ili wanadamu wote twende katika mapito yako. Ee Bwana.

3. Utujalie sisi sote moyo mtulivu ili tupate kulitafakari vema fumbo la ujio wa Mkombozi wetu. Ee Bwana.

4. Uwapokee kwako marehemu wetu F. na wote wanaokujia kila siku makundi makundi, na uwaketishe pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wako wa mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu, umtume Mwanao atuponye katika udhaifu wetu, utujalie imani kubwa na thabiti kama ya yule akida wa Kapernaum, ili hatimaye tufike kwako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.