JUMATATU JUMA 1 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.1:1–6
Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku
hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa mng’ao wa utukufu wake na chapa ya
nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume
wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao. Kwa
maana alimwambia malaika yupi wakati wowote, ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa? Na tena mimi nitakuwa kwake
baba, na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika
wote wa Mungu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.97:1–2,6–7,9 (K)7
1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
(K) Enyi miungu yote, msujuduni Yeye.
2. Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake.
Enyi miungu yote, msujuduni Yeye. (K)
3. Maana Wewe, Bwana, ndiwe uliye juu,
Juu sana kuliko nchi yote;
Umetukuka sana juu ya miungu yote. (K)
SHANGILIO: 1Pet.1:25
Aleluya, aleluya!
Neno la Bwana hudumu hata milele, ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya!
INJILI: Mk1:14-20
Baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema,
Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita
kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana
walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara
wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana
nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao
Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, kwa Ubatizo wetu tumeungama umungu
wa kweli na wa milele na tunaona fahari kuabudu nafsi
tatu za Mungu mmoja zenye utukufu ulio sawa. Basi na
tumwombe Mungu tukisema.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umbariki Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote
wa Kanisa lako. Ee Bwana.
2. Watawala wa nchi na wote wenye mamlaka katika
jamii zetu waige mfano wa manabii katika kutimiza
wajibu zao. Ee Bwana.
3. Sisi sote tujaliwe mng'ao wa utukufu wa Mungu na
chapa ya nafsi yake kwa kushika amri, kuiamini Injili
na kufanya utakaso wa dhambi. Ee Bwana.
4. Utuepushe na tabia ya kuwachokoza, kuwakejeli na
kuwasikitisha wenye matatizo; bali tuwasaidie,
tuwatie moyo na kuwaombea. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapokelewe kwako wapate
kukusujudu pamoja na malaika wako watakatifu. Ee
Bwana.
Ee Mungu unayependa tuyaache yote na kukufuata,
uyapokee maombi yetu haya. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu. Amina.