JUMATATU JUMA 22 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 1Kor.2:1-5
Ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno,
wala kwa hekima. Maana naliazimu nisijue neno lolote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa.
Nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi. Na neno langu na
kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili
za Roho na za nguvu, ili Imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:97-102(K)97
1. Sharia yako naipenda mno ajabu,
Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.
Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu,
Kwa maana ninayo siku zote.
(K) Sheria yako, Ee Bwana, naipenda mno ajabu.
2. Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote,
Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.
Ninao ufahamu kuliko wazee,
Kwa kuwa nimeyashika mausia yako. (K)
3. Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya,
Ili nilitii neno lako.
Sikujiepusha na hukumu zako,
Maana Wewe mwenyewe umenifundisha. (K)
SHANGILIO: Kol.3:16,17
Aleluya, aleluya!
Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote; mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.
Aleluya!
INJILI: Lk.4:16-30
Yesu alienda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama
ilivyokuwa desturi yake, akasimama ilia some. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo,
akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta
kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na
vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.
Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi
wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia
wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake. Wakasema, Huyu siye mwana wa
Yusufu? Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo
yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende hapa pia katika nchi yako mwenyewe.
akasema, Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubalika nchi yake mwenyewe. Lakini,
kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati
mbingu zilipofungwa miaka mitano na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya
hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa
na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila
Naamani, mtu wa Shamu. Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo.
Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa
juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, wajibu wa kuihubiri Injili tuliopewa siku ya
Ubatizo unakabiliwa na changamoto nyingi. Bila msaada
wa Mungu mwenyewe hatutaweza kuutimiza sawa sawa
wajibu huo mkubwa. Tuombe.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Umjalie Baba Mtakatifu wetu F. na wachungaji wote
wa Kanisa lako kuitangaza Injili yako na kuitetea
imani sahihi hasa wanapokabiliwa na upinzani mkali. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wajaliwe kusimamia vema sheria
zinazowapa watu uhuru wa kuabudu na kulitangaza
jina lako. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kulishuhudia fumbo la Pasaka bila
woga katika maisha yetu ya kila siku, ili tupate tuzo
siku ya ufufuko wetu. Ee Bwana.
4. Roho wako Mtakatifu awasaidie wanaohangaika
kutafuta ukweli kwa wahubiri mbalimbali, ili imani
yao isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika
nguvu za Mungu. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu waliolala mauti wafike kwako, wapate
kuishi Nawe milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tufarijiwe na neno lako, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.