JUMATATU JUMA 23 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: 1Kor.5:1-8
Habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe, nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo. Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu; kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu. Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.5:4-6,11(K)8
1. Unawachukia wote watendao ubatili.
Utawaharibu wasemao uongo;
Bwana humzira mwuaji na mwenye hila.

(K) Bwana, uniongoze kwa haki yako.

2. Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya;
Mtu mwovu hatakaa kwako;
Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako. (K)

3. Nao wote wanaokukimbilia watafurahi;
Watapiga daima kelele za furaha.
Kwa kuwa Wewe unawahifadhi,
Walipendao jina lako watakufurahia. (K)

SHANGILIO: Zab.19:8
Aleluya, aleluya!
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya!

INJILI: Lk.6:6-11
Ilikuwa siku ya sabato nyingine Yesu aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza. Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia. Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama. Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza? Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu anatupenda na yupo tayari kutusaidia katika shida zetu. Kwa matumaini hayo, tumwombe.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Askofu wetu F. na Mapadre wote kufurahia mateso katika utume wao, ili uwakili wako waliopewa uwe kweli kwa faida ya watu wako. Ee Bwana.

2. Viongozi wasio wa dini wasiwazuie wachungaji wetu wanaomwonya na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, wapate kumleta kila mtu katika utimilifu wa Mwanao. Ee Bwana.

3. Umjalie kila mmoja wetu kutenda kazi kwa ajili ya neno lako, kwa mfano na msaada wa Kristo Mwanao atendaye kazi kwa nguvu ndani yetu. Ee Bwana.

4. Tunawaombea wakosefu, ili wasijisifie maovu yao; bali waongoke na, wakisha tubu, wawe chachu ya weupe wa moyo na kweli. Ee Bwana.

5. Wagonjwa wetu wajaliwe afya njema, na marehemu wetu wapewe uzima wako wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka tufuate pia roho ya sheria na amri zako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.