JUMATATU JUMA 24 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 1Kor.11:17-26,33
maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki; kwa maana
lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu. Basi mkutanikapo pamoja
haiwezekani kula chakula cha Bwana; kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika
kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au
mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu?
La! Siwasifu kwa ajili ya hayo. Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya
kuwa Bwana Yesu usiku ule alitolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega,
akasema, huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi
hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu;
fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywa
kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate
kula, mngojane.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.40:6-8,16(K)1Kor11:26
1. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja.
(K) Mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.
2. Katika gombo la chuo nimeandikwa,
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
3. Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)
4. Washangilie, wakafurahie,
Wote wakutafutao.
Waupendao wokovu wako
Waseme daima. Atukuzwe Bwana. (K)
SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema: mimi ndimi njia, na ukweli na uzima; mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya Mimi.
Aleluya!
INJILI: Lk.7:1-10
Yesu alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni kwa watu, aliingia Kapernaumu. Na
mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana.
Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa
wake. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno
hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi. Basi Yesu akaenda pamoja
nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia,
Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; kwa hiyo nilijiona
sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona. Kwa maana mimi
nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda,
huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo
alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli
sijaona Imani kubwa namna hii. Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa
ni mzima.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu wapendwa, Mungu yupo tayari kuwasaidia wote
wenye shida wanaomwendea kwa imani na moyo
mnyofu. Kwa hiyo, tumwombe.
Kiitikio:Upokee ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu na Mapadre
waimarishwe katika kuhubiri, kufundisha na kufanya
utume mbalimbali katika imani ya kweli. Ee Bwana.
2. Utujalie kufanya dua, sala, maombezi na shukrani
kwa ajili ya wafalme, wote wenye mamlaka na watu
wote, tupate kuishi maisha ya utulivu na amani. Ee Bwana.
3. Katika tafakari zetu, utujalie fursa ya kukutana na
Wewe Mungu, tupate kuponywa roho zetu. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wote wanaofika kanisani, ili
wapaheshimu mahali patakatifu na kupatumia kwa
malengo yaliyokusudiwa, kwa wokovu wa watu na
kwa sifa na utukufu wako. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu waliokuamini, uwajalie maisha
mapya ya ufufuko na uzima huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tuwe na imani thabiti katika uwezo
wako wa kuponya roho na mwili, uyapokee maombi yetu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.