JUMATATU JUMA 25 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Mit.3:27-34
Mwanangu, Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.
Usimwambie jirani yako, nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; nawe unacho kitu kile karibu
nawe. Usiwaze mabaya juu ya jirani yako, ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama.
Usishindane na mtu bila sababu, ikiwa hakukudhuru kwa lolote. Usimhusudu mtu mwenye jeuri,
wala usiichague mojawapo ya njia zake. Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, bali siri yake
ni pamoja na wanyofu. Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, bali huibariki maskani ya wenye
haki. Hakika yake huwadharau wenye dharau, bali huwapa wanyenyekevu neema.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.15(K)1
1. Ni nani atakayefanya maskani yake
Katika kilima chako kitakatifu.
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki, asemaye kweli kwa moyo wake
Asiyesingizia kwa ulimi wake.
(K) Mtu aendaye kwa ukamilifu, atafanya maskani yake,
katika kilima chako kitakatifu.
2. Asiyemtendea mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana.
Ingawa ameapa kwa hasara yake,
Hayabadili maneno yake. (K)
3. Hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele. (K)
SHANGILIO: Yak.1:18
Aleluya, aleluya!
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli,
tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya!
INJILI: Lk.8:16-18
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo,
au kuiweka uvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Kwa
maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana
na kutokea wazi. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye
na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu ambaye furaha yako imekuwa daima pamoja
na wanadamu, tunakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie viongozi wetu wa Kanisa kuyaona matunda
ya kazi zao za kitume, wapate kutiwa moyo na ari ya
kuliongoza kundi lako katika njia ya imani. Ee Bwana.
2. Uamshe ndani ya watawala wa dunia tabia ya
kuthamini uwepo wako wa kimungu, na kuwapa watu
wako uhuru wa kukuabudu Wewe. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kuwa wakarimu kwa wenye shida
ili, kwa huduma zetu na upendo wetu kwao, wapate
kukutana nawe uliye mpaji wa vyote. Ee Bwana.
4. Tunajiombea wenyewe dhidi ya watu jeuri, wakaidi
na waovu; ili waache machukizo na njia zao
mbaya; sisi tupate amani na usalama. Ee Bwana.
5. Uwajalie marehemu wetu waione nuru yako isiyofifia
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu ambaye kwako hakuna lililositirika ambalo
halitafunuliwa, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.