JUMATATU JUMA 26 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Ayu.1:6-22
Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani
naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza, Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu
Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku
humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa
hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na uelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana
na uovu. Ndipo shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe
hukumzingira kwa ukingo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi
za mikono yake umezibariki, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako
sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. Bwana akamwambia shetani,
Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye
mwenyewe. Basi shetani akatoka mbele za uso wa Bwana. Ilitukia siku moja hao wanawe na binti
zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, mjumbe akamfikilia
Ayubu na kumwambia, Hao ng’ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao; mara
Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam wamewaua hao watumishi kwa makali ya
upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena,
akatokea mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo,
na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo
alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu,
wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi
peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na
mwingine, na kusema, wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu
yao mkubwa; mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba
pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi
tu, kukuletea habari. Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake,
na kuanguka na nchi, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi,
nami nitarudi tena huko nili uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na
libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.17:1-3,6-7(K)6
1. Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila.
(K) Utege sikio lako ulisikie neno langu.
2. Hukumu yangu na itoke kwako,
Macho yako na yatazame mambo ya adili.
Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku,
Umenihakikisha usione neno. (K)
3. Ee Mungu nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
Dhihirisha fadhili zako za ajabu,
Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia. (K)
SHANGILIO: Zab.119:28,33
Aleluya, aleluya!
Unitie nguvu sawa sawa na neno lako, Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya!
INJILI: Lk.9:46-50
Wanafunzi walianza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao. Naye Yesu alipotambua
mawazo ya mioyo yao, alitwaa mtoto mdogo akamweka karibu naye, akawaambia, Yeyote atakayempokea
mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na yeyote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma.
Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa. Yohane akajibu akamwambia; Bwana
mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa asababu hafuatani na sisi. Yesu
akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa imani na matumaini tumwombe Mungu
aliye mmoja katika Utatu Mtakatifu tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwe pamoja na Askofu wetu F. na Mapadre wetu
wote, katika utumishi wao mtakatifu wa kumleta na
kumtambulisha Mwanao Yesu Kristo kwa watu. Ee Bwana.
2. Kwa kuwa raslimali zote za taifa zimo mikononi
mwa viongozi wa nchi, uwajalie kuzitumia
iwapasavyo, bila kuingilia maslahi ya watu binafsi. Ee Bwana.
3. Wazee wote katika jamii zetu wajaliwe kudumu katika
imani sahihi waliyoipokea, na wairithishe imani hiyo
pamoja na mila na desturi njema kwa watoto na
wajukuu wao. Ee Bwana.
4. Utujalie sisi sote unyenyekevu na bidii ya kuhudumiana,
tupate kulipokea na kuliishi neno lako kadiri
linavyodai, bila kujitakia makuu. Ee Bwana.
5. Uwarehemu marehemu wetu na kuwapa uzima wa
milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.