JUMATATU JUMA 27 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Gal.1:6-12
Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo. Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.111:1-2,7-10(K)5
Aleluya.
1. Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu,
Ukawafunulia watoto wachanga.

(K) Alikumbuka agano lake milele.

2. Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,
Maagizo yake yote ni amini.
Yamethibitika milele na milele,
Yamefanywa katika kweli na adili. (K)

3. Amewapelekea watu wake ukombozi,
Ameamuru agano lake liwe la milele.
Jina lake ni takatifu la kuogopwa.
Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima,
Wote wafanyao hayo wana akili njema,
Sifa zake zakaa milele. (K)

SHANGILIO: 2Kor.5:19
Aleluya, aleluya!
Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya!

INJILI: Lk.10:25-37
Mwanasheria mmoja alisimama akamjaribu Yesu, akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na lipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.