JUMATATU JUMA 28 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Gal.4:22-24,26-27,31-5:1
Imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili. Mmoja alikuwa mjakazi na mwingine alikuwa
muungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa muungwana kwa ahadi. Mambo haya
husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, mmoja kutoka Sinai, lizaalo kwa
utumwa, ambalo ni hajiri. Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana naye ndiye mama yetu sisi. Kwa
maana imeandikwa, furahi wewe uliye tasa, usiye zaa; paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu: maana
watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi kuliko huyo aliye na mume. Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto
wa mjakazi bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana. Katika ungwana huo Kristo alituandikia huru; kwa
hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.113:1-7(K)2
Aleluya
1. Enyi watumishi wa Bwana sifuni
Lisifuni jina la Bwana
Jina la Bwana lihimidiwe
Tangu leo na hata milele.
(K) Jina la bwana lihimidiwe milele.
2. Toka mawio ya jua hata machweo yake
Jina la bwana husifiwa
Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote
Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K)
3. Ni nani aliye mfano wa bwana
Mungu wetu aketiye juu
Anyenyekeaye kutazama
Mbinguni na duniani?
Humwinua mnyonge kutoka mavumbini
Na kumpandisha masikini toka jaani. (K)
SHANGILIO: Zab.119:34
Aleluya, aleluya!
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako. Nitaitii kwa moyo wangu wote,
Aleluya!
INJILI: Lk.11:29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta
ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa
Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya
hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka
nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi
watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao
walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Yesu Kristo ambaye ni wa ukoo wa Daudi na Mkuu
kuliko Sulemani, alijidhihirisha kuwa ni Mwana wa
Mungu kwa roho ya utakatifu na kwa ufufuko wake
kutoka wafu. Tumwombe Mungu tukisema:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Viongozi wote wa Kanisa wasichoke kuihubiri Injili,
ili wengi zaidi wapate kuamini na kubatizwa kwa jina
la Mwanao Yesu Kristo. Ee Bwana.
2. Uwaonye watu wasiomkiri Mwanao Yesu Kristo,
wapate kuishuhudia hekima yake na ishara zitokazo
kwako. Ee Bwana.
3. Umjalie kila mmoja wetu kutunza neema ya utakatifu
tuliyopewa siku ya Ubatizo, tupate kustahili wokovu
uliokamilishwa kwa fumbo la Pasaka. Ee Bwana.
4. Wakristo wenzetu wanaokosa uungwana na
kuyumbayumba katika imani, wamrudie Kristo
aliyewaandika huru; wasimame imara, wala
wasinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Ee Bwana.
5. Marehemu wanaongojea huruma yako wapokelewe
huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.