JUMATATU JUMA 29 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Efe.2:1-10
Mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida
ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye zake sasa katika
wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu,
tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yenu watoto wa hasira kama na hao
wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata
wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani mmeokolewa
kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo
Yesu. Ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu
sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya Imani; ambayo hiyo haikutokana
na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu
kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza
ili tuenende nayo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.100(K)3
1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba.
(K) Ndiye aliyetuumba, na sisi tu watu wake.
2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
3. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake. (K)
4. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)
SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe,
bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya!
INJILI: Lk.12;13-21
Mtu mmoja katika mkutano alimwambia Yesu, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.
Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia,
Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.
Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza
moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya
hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote
na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa
miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu
wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye
nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.
--------------
--------------
MAOMBI
Kwa vile pendo la Mungu limekwisha kumiminwa
mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu, tumehesabiwa haki
pasipo mastahili. Tumsifu na kumtukuza Mungu
tukisema:-
Kiitikio: Utukuzwe, Ee Mungu.
1. Kwa kuwa umelijalia Kanisa lako Maaskofu na
apadre ambao wamehesabiwa haki ya kuushiriki
ukuhani wa Mwanao Yesu Kristo.
2. Kwa kuwa hata viongozi wa serikali ni kazi yako,
wameumbwa ili watende matendo mema, ambayo
tokea mwanzo uliyatengeneza ili tuende nayo.
3. Kwa kuwa watu wote duniani wamehesabiwa haki ya
kuwa wazao wa Ibrahimu aliye baba yetu wa Imani.
4. Kwa kuwa sisi tunaokuamini tulipata kuhesabiwa haki
kwa Fumbo Kuu la Pasaka, lilitotimizwa na
Mwanao Mpenzi Yesu Kristo.
5. Kwa kuwa hata ndugu zetu marehemu wamehesabiwa
haki, wanaombewa na sisi tulio bado hai hapa
duniani, ili wapewe uzima wa milele huko mbinguni.
Ee Mungu unayetaka tujitajirishe kwako, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.