JUMATATU JUMA 2 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.5:1-10
Kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo
Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua
na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama
kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi.
Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. Vivyo
hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu,
Mimi leo nimekuzaa. kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani wa milele Kwa mfano wa Melkizedeki. Yeye,
siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja
na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza
kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa
watu wote wanaomtii; kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.110:1-4 (K)4
1. Neno la Bwana kwa Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume,
Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.
(K) Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki.
2. Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako.
Uwe na enzi kati ya adui zako; (K)
3. Watu wako wanajitoa kwa hiari,
Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu,
Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako. (K)
4. Bwana ameapa, Wala hataghairi,
Ndiwe kuhani hata milele,
Kwa mfano wa Melkizedeki.(K)
SHANGILIO: Ebr.4:12
Aleluya, aleluya,
Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu,
tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho.
Aleluya.
INJILI: Mk.2:18-22
Siku moja wanafunzi wake Yohane na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia,
Kwani wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?
Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda
wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja watakapoondolewa
bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile. Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi
kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka
huzidi. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya
itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika
viriba vipya.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa twakiri kwamba vipaji vyote vyatoka
kwa Mungu, tuombe tukisema.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwakirimie Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu na
Mapadre wote neema ya ukuhani ule wa Mwanao
Yesu Kristo. Ee Bwana.
2. Viongozi wote katika jamii zetu wavuviwe roho ya
kuwa wacha Mungu. Ee Bwana.
3. Wote wanaokukiri Wewe Mungu Baba, Mwana na
Roho Mtakatifu wazielekeze daima sala zao kwako
Wewe uwezaye kuwaokoa na kuwatoa katika mauti. Ee Bwana,
4. Uwajalie watu wote, wakubwa kwa wadogo, kukumbuka
daima kuwa utii ni bora kuliko sadaka. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wajaliwe wokovu wa milele. Ee Bwana.
Utujalie hayo tuliyokuomba, Ee Mungu, kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.