JUMATATU JUMA 31 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Flp.2:1.4
Ikiwako faraja yoyote katika Kristo, yakiwako matulizo yoyote ya mapenzi, ukiwako ushirika
wowote wa Roho, ikiwako huruma yoyote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja,
wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja. Msitende neno lolote kwa kushindana wala
kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.
Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.131
1. Bwana, moyo wangu hauna kiburi,
Wala macho yangu hayainuki.
Wala sijushughulishi na mambo makuu,
Wala na mambo yashindayo nguvu zangu.
(K) Moyo wangu uwe na amani kwako, Ee Bwana.
2. Hakika nimeituliza nafsi yangu,
Na kuinyamazisha.
Kama mtoto aliyeachishwa
Kifuani mwa mama yake;
Ndivyo roho yangu ilivyo kwangu. (K)
3. Ee Israeli, umtarajie Bwana,
Tangu leo na hata milele. (K)
SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya!
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya!
INJILI: Lk.14:12-14
Yesu alimwambia yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki
zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika
wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa
heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu aliye mkarimu na mwenye huruma daima
yupo tayari kusikiliza sala zetu. Na hivi tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wa Kanisa wajaliwe kuwahubiria waamini
wao neno lako kadiri ya alama za nyakati, na
kubainisha imani halisi ya watu wako. Ee Bwana.
2. Viongozi wa serikali na taasisi zake wawahudumie
watu kwa unyenyekevu; wakiwaangalia kwanza
wenye shida. Ee Bwana.
3. Kwa kuishi na kufanya kazi pamoja na waamini
wenye imani safi, wote waliokuasi Wewe Mungu
wajaliwe wongofu na maisha ya fadhila. Ee Bwana.
4. Sisi sote tujaliwe moyo wa huruma na ukarimu kwa
wenye shida, ili nao waonje uwepo wako na rehema
yako. Ee Bwana.
5. Uwarehemu ndugu zetu marehemu na kuwashirikisha
utukufu wa ufufuko wa wenye haki huko mbinguni.
Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetuahidia malipo ya ukarimu katika
ufufuko wa wenye haki, uyapokee maombi yetu. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.