JUMATATU JUMA 32 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Tit.1:1-9
Paulo, mtumwa wa Mungu, na mtume wa Yesu Kristo; kwa ajili ya Imani ya wateule wa Mungu, na
ujuzi wa kweli ile iletayo utauwa; katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza
kusema uongo aliuahidi tangu milele; akalifunua neno lake kwa majira yake katika ule ujumbe
niliowekewa amana mimi kwa amri ya Mwokozi wetu Mungu; kwa Tito, mwanangu hasa katika Imani
tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi
wetu. Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika
kila mji kama vile nilivyokuamuru; ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana
watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii. Maana imempasa askofu awe mtu
asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipendekeza nafsi yake, asiwe
mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu; bali awe mkaribishaji,
mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile
neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye
uzima, na kuwashinda wenye kupinga.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:1-6(K)6
1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.
2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)
3. Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
SHANGILIO: 1Sam.3:9,Yn.6:68
Aleluya, aleluya!
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia: wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya!
INJILI: Lk.17:1-6
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja
kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusaga lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini,
kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni. Kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu
msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu,
msamehe. Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee Imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na Imani kiasi
cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka ukapandwe baharini, nao ungewatii.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, uliyetujalia zawadi ya ufunuo mpana zaidi
kuliko ule wa mitume, twakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Ili Baba Mtakatifu F.,
Askofu wetu F. na wakleri
wote wazidi kuwaonya watu wako dhidi ya
usababishaji makwazo; na kuhimiza upendo,
hekima na haki. Ee Bwana.
2. Ili taifa lako lipate daima viongozi wenye sifa
njema; wakaribishaji na wema, wenye kiasi na haki,
watakatifu, wenye imani sahihi, na wenye uwezo
wa kufundisha watu na kukemea maovu. Ee Bwana.
3. Ili waamuzi wa dunia wapende haki, watafakari habari
zako Bwana kwa moyo mwema, na kukutafuta katika
unyofu wa moyo. Ee Bwana.
4. Ili tujaliwe hekima yako ya kimungu, tupate kuwaza,
kusema na kutenda yakupendezayo Wewe na jirani zetu. Ee Bwana.
5. Ili marehemu wetu wafutiwe dhambi zao na kupewa
heri ya milele katika ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayejifunua kwao wakuaminio, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.