JUMATATU JUMA 33 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Ufu.1:1-4;2:1-5
Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaoneshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa malaika akamwonesha mtumwa wake Yohane: aliyelishuhudia Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu Kristo, yaani, mambo yote aliyoyaona. Heri asomaye na wao wayasikiao yote aliyoyaona. Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu. Yohane, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia: Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi. Nilisikia Bwana ananiambia: Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu. Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakin nina neno juu yako, na ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulioanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.1:1-4,6(K)Ufu2:7
1. Heri mtu yule asiyekwenda,
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.

(K) Yeye ashindaye, nitampa matunda ya mti wa uzima.

2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

3. Sivyo walivyo wasio haki;
Nao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni,
Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki. (K)

SHANGILIO: Mt.4:4
Aleluya, aleluya!
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Aleluya!

INJILI: Lk.18:35-43
Yesu alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; Imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu Baba, umetuletea neno lenye kutuandaa kwa siku ya mwisho. Hivyo, huku tukikushukuru, tunakuomba tukisema.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Upokee shukrani zetu kwa kuwa Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wengi wa Kanisa wanafanya jitihada za kuieneza imani aliyotuachia Mwanao. Ee Bwana.

2. Uwakinge waamini wako na chachu ya kipagani, ili walishike agano lako takatifu, na kukutumainia Wewe katika maisha yote. Ee Bwana.

3. Utujalie imani thabiti kama ya yule kipofu wa Yeriko, tupate kuponywa udhaifu wetu na kuona njia iendayo kwako. Ee Bwana.

4. Kwa namna ya pekee umsaidie kila aliyeuacha upendo wake wa kwanza, umkumbushe ni wapi alikoanguka; apate kutubu na akayafanye matendo ya kwanza. Ee Bwana.

5. Imani waliyokuwa nayo ndugu zetu marehemu iwaponye na dhambi wapate kuingia kwako mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayewapokea na kuwaponya wote wanaokujia kwa moyo mnyofu na imani thabiti, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.