JUMATATU JUMA 34 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Ufu.14:1-5
Mimi, Yohane, niliona, na tazama, huyo Mwanakondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia
na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika
vipaji vya nyuso zao. Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama
sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakavipiga
vinubi vyao; na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne,
na wale wazee; wala hapana mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale mia na arobaini na nne
elfu, walionunuliwa katika nchi. Hawa ndio wasiotiwa unajisi pamoja na wanawake, kwa maana ni
bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwanakondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko
kwa Mungu na kwa Mwanakondoo. Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:1-6(K)6
1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.
2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
Wala hakuapa kwa hila. (K)
3. Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wake, Ee Bwana wa Yakobo. (K)
SHANGILIO: Ebr.4:12
Aleluya, aleluya!
Neno la Mungu li hai tena lina nguvu, li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya!
INJILI: Lk.21:1-4
Yesu aliinua macho yake akawaona matajiri wakitia sadaka zao katika sanduku la hazina.
Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili. Akasema, Hakika nawaambieni, hao wote
walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote
alivyokuwa navyo.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, tumwombe Mungu anayependa tujitoe kabisa bila kujibakiza kwa ajili
ya ufalme wake tukisema.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Baba Mtakatifu F. na wakubwa wote wa Kanisa, wazidi
kujitoa bila kujibakiza katika kuilinda na kuitetea imani yetu kwako. Ee Bwana.
2. Wafalme na wote wenye mamlaka wasijitwalie madaraka ya kimungu, wala
kuwapotosha watu uliowaumba kwa ajili ya kukutumikia Wewe. Ee Bwana.
3. Watu wote duniani wajaliwe kukutii na kukupa heshima na sadaka ya juu
kabisa. Ee Bwana.
4. Kwa neema yako, tujaliwe kujiandaa vema kukijongea kiti chako cha enzi,
kwa usafi wa moyo na bila waa lolote. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wapewe rehema yako na uzima wa milele huko
mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, uyapokee maombi yetu haya na hata yale ambayo hatukuyataja. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.