JUMATATU JUMA 3 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Hes.24:2-7, 15-17
Siku zile Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kabila; roho ya Mungu ikamjia.
Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; Asema,
yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho;
Mahema yako ni mazuri namna gani, Ee Yakobo, Maskani zako, Ee Israeli! Mfano wa bonde zimetandwa, Mfano
wa bustani kando ya mto, Mfano wa mishubiri aliyoipanda Bwana, Mfano wa mierezi kando ya maji. Maji
yatafurika katika ndoo zake, Na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake ataadhimishwa
kuliko Agagi, Na ufalme wake utatukuzwa. Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema,
Yule mtu aliyefumbwa macho asema, Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye
Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, Namwona, lakini si sasa;
Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli;
WIMBO WA KATIKATI: Zab.25:4-6,7b-9
1. Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha.
Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu,
Nakungoja Wewe mchana kutwa. (K)
(K) Ee Bwana unijulishe njia zako.
2. Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana kwa ajili ya wema wako. (K)
3. Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)
Shangilio: Zab.85:7
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, utuoneshe rehema zako, utupe wokovu wako.
Aleluya.
INJILI: Mt.21:23-27
Siku ile Yesu alipokwisha kuingia hekaluni, wakuu wa makuhani na wazee wa watu wakamwendea alipokuwa
akifundisha, wakasema, Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii? Yesu akajibu
akawaambia, Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa amri gani ninatenda
haya. Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Wakahojiana wao kwa wao, wakisema,
Tukisema, Ulitoka mbinguni, atatuambia, Mbona basi hamkumwamini? Na tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, twaogopa
mkutano; maana watu wote wamwona Yohana kuwa ni nabii. Wakamjibu Yesu wakasema, Hatujui. Naye akawaambia,
Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa amri gani ninatenda haya.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, Bwana yu mwema, mwenye adili, kwani huwafundisha wenye dhambi njia, na wenye upole
huwaongoza katika hukumu. Tumwombe ili atuoneshe rehema yake.
Kiitikio: Twaomba rehema yako.
1. Utuongezee wachungaji bora katika Kanisa lako, ili watujulishe njia yako na kutufundisha mapito yako.
Ee Bwana.
2. Utuongoze katika kweli yako katika ulimwengu huu geugeu. Ee Bwana.
3. Utuimarishe ili tuishi kadiri ya imani yetu ya Ubatizo mpaka siku ya ujio wa Mkombozi wetu. Ee Bwana.
4. Ndugu zetu marehemu F. na wote walioaga dunia katika hali ya neema
wapokelewe katika ufalme wa mbinguni. Ee Bwana.
Ee Bwana, tunakiri kwamba vyote vimetoka kwako, hata Mkombozi tunayemtazamia. Uongoze mawazo, maneno
na matendo yetu kwenye wokovu wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.