JUMATATU JUMA 3 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.9:15,24-28
Kristo ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya
agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele. Kwa sababu Kristo hakuingia katika
patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa,
aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu
aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara
nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati,
amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara
moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue
dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-6 (K)1
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
3. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
4. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)
SHANGILIO: 2Tim.1:10
Aleluya, aleluya,
Mwokozi wetu Yesu Kristu alibatili mauti,
na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya.
INJILI: Mk.3:22-30
Waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa
pepo. Akawaita, akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani? Na ufalme ukifitinika
juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba
hiyo haiwezi kusimama. Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama,
bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake,
asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake. Amin, nawaambia, Dhambi
zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho
Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele, kwa vile walivyosema, Ana
pepo mchafu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu Baba anayetukuka katika
Utatu Mtakatifu tukisema:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Makuhani wako wazidi kuutumia uwezo waliopewa
na Kristo wa kuondolea dhambi za watu. Ee Bwana.
2. Viongozi wote wa jamii zetu wajibidishe katika
kuzitatua kwa wakati kero zinazowakabili wale
wanaowaongoza. Ee Bwana.
3. Utuongezee moyo wa ushirikiano na wakuu wetu
na wote wenye mamlaka yatokayo kwako, ili
mapenzi yako yatimizwe kwa wakati uliokusudiwa.
Ee Bwana.
4. Utuepushe sisi sote na dhambi wala tusidiriki
kumkufuru Roho wako Mtakatifu. Ee Bwana.
5. Uwasamehe dhambi zao ndugu zetu marehemu
wapate kutawala nawe milele huko mbinguni. Ee
Bwana.
Ee Bwana Mungu, tunakuomba utujalie hayo yote. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.