JUMATATU JUMA 4 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.11:32-40
Ndugu zangu niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na
Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme,
walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na
makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza
majeshi ya wageni. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya
hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka
na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno,
walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi;
walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao),
walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo
ya nchi. Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi; kwa
kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo
sisi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.31:19-23 (K)24
1. Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako
Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao
Mbele ya wanadamu!
(K) Iweni hodari, mpige moyo konde,
nyinyi nyote mnaomngoja Bwana.
2. Utawasitiri na fitina za watu
Katika sitara ya kuwapo kwako;
Utawaficha katika hema
Na mashindano ya ndimi. (K)
3. Bwana ahimidiwe;
kwa maana amenitendea
Fadhili za ajabu katika mji wenye boma. (K)
4. Nami nalisema kwa haraka yangu,
Nimekatiliwa mbali na macho yako;
Lakini ulisikia sauti ya dua yangu Wakati nilipokulilia. (K)
5. Mpendeni Bwana, Ninyi nyote mlio watauwa wake.
Bwana huwahifadhi waaminifu,
Humlipa atendaye kiburi malipo tele. (K)
SHANGILIO: Yn.15:15
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema:
Siwaiti tena watumwa,
lakini ninyi nimewaita rafiki,
kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
INJILI: Mk.5:1–20
Yesu na wanafunzi wake walifika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. Na alipokwisha kushuka
chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; makao yake yalikuwa
pale makaburini; wala hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; kwa sababu
alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja
zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Na siku zote, usiku na mchana, alikuwako
makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakatia kwa mawe. Na alipomwona Yesu kwa mbali,
alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa
Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu
huyu. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi. Akamsihi sana
asiwapeleke nje ya nchi ile. Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha. Pepo
wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao. Akawapa ruhusa. Wale pepo
wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni,
wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini. Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari
mjini na mashamba. Watu wakatoka walione lililotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo,
ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa. Na wale
waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe.
Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao. Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo
akamsihi kwamba awe pamoja naye; lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako,
kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu.
Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote
wakastaajabu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tumwombe Mungu aliyejifunua hata katika
Waamuzi na Manabii wake watakatifu tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwajalie Baba Mtakatifu wetu F. Maaskofu na
viongozi wote wa Kanisa ujasiri katika kuitangaza
Habari Njema kokote wanakohitajika. Ee Bwana.
2. Wote wenye madaraka serikalini na kwenye taasisi
zote, wajaliwe neema na nguvu ya kutetea haki
za wanyonge, kama walivyofanya Waamuzi na
manabii. Ee Bwana.
3. Kila mwana jumuiya ya kikristo, ajaliwe bidii
ya kutimiza kiaminifu wajibu zake zote za kijamii na
za kidini, kadiri ya nafasi na uwezo wake. Ee
Bwana.
4. Utujalie Roho wako ili daima tuweze kufanya
maamuzi ya busara, tuache umwagaji damu isiyo
na hatia na kukataa dhambi nyingine zote. Ee
Bwana.
5. Marehemu wetu washirikishwe utukufu ule wa Baba
na Mwana na Roho Mtakatifu. Ee Bwana.
Ee Mungu uliye nguvu na tegemeo letu, upende kuyapokea
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.