JUMATATU JUMA 6 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.4:1-15,25
Adamu alimjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana.
Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.
Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa
wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini
hakumakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. Bwana akamwambia
Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali?
Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini
akamwambia Habili nduguye, twende uwandani. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili
nduguye, akamwua. Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi
wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.
Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono
wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoto na mtu asiye na kikao duniani. Kaini
akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikalia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa
ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa
kila anionaye ataniua. Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo yeyote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi
mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. Adamu akamjua mke wake tena; akazaa
mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa
Habili; kwa sababu Kaini alimwua.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.50:1,8,16–17,20–21. (K)14
1. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
Toka maawio ya jua hata machweo yake.
Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
(K) Umtolee Mungu dhabihu za kushukuru.
2. Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia,
Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
3. Umekaa na kumsengenya ndugu yako,
Na mwana wa mama yako umemsingizia.
Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza,
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
Walakini nitakukemea;
Nitayapanga hayo mbele ya macho yako. (K)
SHANGILIO: 1Sam.3:9
Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia:
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.
INJILI: Mk.8:11–13
Walitokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana na Yesu; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni;
wakimjaribu. Akaugua rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni,
Hakitapewa ishara kizazi hiki. Akawaacha akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng’ambo.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, dhambi zina madhara makubwa kwa binadamu
na humwudhi hata Mungu. Tuombe neema yake dhidi ya
dhambi tukisema:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Uwaimarishe wachungaji wetu katika kuhubiri upendo,
ili watu wako waepukane na wivu, chuki na
tamaa mbaya. Ee Bwana.
2. Wote wanaosimamia sheria watoe hukumu za haki
kwa raia wao, ili kudumisha haki, amani na
usawa. Ee Bwana.
3. Utuepushe sisi sote na mawazo, maneno na matendo
mabaya kwani yanasababisha hata mauaji kwa wenzetu
hata kwa namna tusizozijua. Ee Bwana.
4. Utujalie kukumbuka kuwa majaribu ya imani yetu
ni fursa ya kuleta saburi, tupate kuwa wakamilifu
na watimilifu bila kupungukiwa na neno. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na
kupokelewa kwako mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, utujalie hayo na hata yale tusiyothutu kuomba.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.