JUMATATU JUMA 7 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Ybs.1:1–10
Hekima yote yatoka kwa Bwana, nayo yakaa kwake hata milele. Nani awezaye kuhesabu mchanga wa habari na matone ya mvua na siku za milele? Nani awezaye kutafuta kimo cha mbingu na upana wa dunia na kina cha bahari? Hekima iliumbwa kabla ya vitu vyote, na ufahamu wa busara tangu milele. Nani aliyefunuliwa shina la hekima? Nani aliyejua mashauri yake merevu? Yuko mmoja aliye na hekima, naye yu wa kuogopwa sana, ameketi katika kiti chake cha enzi. Bwana ndiye aliyeiumba na kuiona na kuihesabu, na kumwaga juu ya kazi zake zote. Ina wote wenye mwili kama aitoavyo, na wale wampendao amewapa kwa wingi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.93:1–2,5 (K)1
1. Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
Bwana amejivika, na kujikaza nguvu.

(K) Bwana ametamalaki, amejivika adhama.

2. Naam, ulimwengu umethibitika isitikisike;
Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani;
Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K)

3. Shuhuda zako ni amini sana;
Utakatifu ndio uifaao nyumba yako,
Ee Bwana, milele na milele. (K)

SHANGILIO: Zab.27:11
Aleluya, aleluya!
Ee Bwana, unifundishe njia yako,
na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya!

INJILI: Mk.9:14-29
Yesu na Petro na Yakobo na Yohane walipowafikia wanafunzi, waliona makutano mkuu wakiwazunguka, na waandishi wakijadiliana nao; mara mkutano wote walipomwona walishangaa, wakamwendea mbio, wakamsalimu. Akawauliza, Mnajadiliana nini nao? Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu; na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze. Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Mleteni kwangu. Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini; akagaagaa. Akitokwa na povu. Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, tangu utoto. Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwamngamize; lakini ukiweza neno lolote, utuhurumie, na kutusaidia. Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye. Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu. Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua; naye akasimama. Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lolote, isipokuwa kwa kuomba.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, huku tukikiri umungu wako mmoja katika nafsi tatu, twaja mbele yako na kukuomba.

Kiitikio: Utupe neema yako:
1. Uwafunulie viongozi wetu wa Kanisa shina la hekima wapate kutimiza mapenzi yako kadiri ya mashauri yako merevu. Ee Bwana.

2. Uwajalie wote wenye mamlaka kukukiri Wewe kuwa ndiwe Mungu mmoja, mwenye hekima ya juu kabisa na wa kuogopwa sana. Ee Bwana.

3. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, utujalie hekima yako sisi sote tukupendao. Ee Bwana.

4. Utuongezee imani, tupate kumkimbilia kwa sala Mwanao, Yesu Kristo, kwani yupo daima tayari kuchukuliana nasi. Ee Bwana.

5. Kwa huruma yako, wagonjwa na wenye pepo wapone; na marehemu wetu wapate uzima wa milele. Ee Bwana.

Ee Mungu, kwa imani thabiti kwako, yote yawezekana. Utujalie hayo yote kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.