JUMATATU JUMA 8 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO: YbS.17:24-29
Hata hivyo huwajalia wale watubuo kurudi, na wao wanaopotewa na saburi kuwafariji. Basi umrudie Bwana
na kuacha dhambi; omba dua yako mbele za uso wake na kupunguza kikwazo; umgeukie tena Yeye Aliye juu,
uyageze maovu, uyakiri yaliyo machukizo. Yaani, Mungu anayo ridhaa gani kwao wanaopotea? ila kwao
wanaoishi na kumtolea shukrani. Shukrani hukoma kutoka kwa wafu, kama kutoka kwake yeye asiyekuwapo;
bali mwenye uzima na afya atamhimidi Bwana, Ee ajabu ya wingi wa rehema za Bwana, na ya masamaha yake
kwao wanaomgeukia!
WIMBO WA KATIKATI: Zab.12:1-2,5-7 (K)11
1. Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makosa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu.
Ambaye rohoni mwake hamna hila.
(K)Mfurahieni Bwana, shangilieni, enyi wenye haki.
2. Nalikujulisha dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu. (K)
3. Kwa hiyo kila mtu mtauwa
Akuombe wakati unapopatikana.
Hakika maji makuu yafurikapo,
Hayatamfikia yeye.
Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso,
utanizungusha nyimbo za wokovu. (K)
SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, ee Yerusalemu,
huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya!
INJILI: Mk.10:17-27
Yesu alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza,
Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita
mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie
uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika
tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja, Enenda
ukauze ulivyo navyo vyote. Uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.
Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika
ufalme wa Mungu! Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi
ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi ngamia kupenya katika
tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu, Nao wakashangaa mno, wakimwambia,
Ni nani, basi, awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa
Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kuingia katika ufalme wa Mungu si rahisi; kwani
kuna vikwazo vingi. Tumwombe Mungu atusaidie.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umzidishie Askofu wetu F. neema ya kuzitambua
shida za watu wake na kuzitatua kwa wakati na kadiri
ya mazingira. Ee Bwana.
2. Uwajalie matajiri moyo wa huruma kwa maskini na
kuwasaidia kadiri ya mapenzi yako. Ee Bwana.
3. Utusaidie sisi sote kujipatanisha nawe na jirani zetu,
na utupe neema ya kukusudia kuacha dhambi kwa
dhati kabisa. Ee Bwana.
4. Utulinde kwa nguvu yako ya kimungu kwa njia ya
imani; hata tupate wokovu ulio tayari kufunuliwa
wakati wa mwisho. Ee Bwana.
5. Uwajalie afya wagojwa wetu; na marehemu wetu
wapate uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu Mtukufu ambaye kwako yote yawezekana,
utujalie hayo na hata yale ambayo hatukuyataja. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.