KUZALIWA BWANA
25 DESEMBA



MASOMO MISA YA ALFAJIRI
ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.9:2,6; Lk.1:33
Nuru itatuangazia leo, maana kwa ajili yetu Bwana amezaliwa; naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu, Mungu, Mfalme wa amani, Baba wa milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.

Utukufu husemwa

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, tunakuomba utujalie ili, maadamu tunaangaziwa na mwanga mpya wa Neno wako aliyetwaa mwili, fumbo linalomulika kwa imani moyoni mwetu lidhihirishwe katika matendo yetu. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa 62:11-12
Tazama Bwana ametangaza habari mpaka mwisho wa dunia, Mwambieni binti Sayuni, Tazama, wokovu wako unakuja; Tazama, thawabu yake i pamoja naye, Na malipo yake yako mbele zake. Nao watawaita, Watu watakatifu, Waliokombolewa na Bwana; Nawe utaitwa, Aliyetafutwa, Mji usioachwa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 97:1,6,11-12
1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi
Mbingu zimetangaza haki yake.
Na watu wote wameuona utukufu wake.

(K) Mwangaza utatung'aria leo: Kwa maana Mwana amezaliwa kwetu.

2. Nuru imemzukia mwenye haki
Na furaha wanyofu wa moyo.
Enyi wenye haki mfurahieni Bwana,
Na kulishukuru jina lake takatifu. (K)

SOMO 2: Tit.3:4-7
Wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.

SHANGILIO: LK.2:14
Aleluya, aleluya!
Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Lk.2:15-20
Ikawa malaika walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.

Nasadiki husemwa. Wote hupiga magoti yasemwapo maneno Akapata mwili ... akawa mwanadamu.

MAOMBI
Ndugu zangu, tumchangamkie Kristo aliyeshangiliwa na Malaika alipozaliwa Betlehemu. Tumwombe tukisema: Utujalie amani!

1. Ulijalie amani Kanisa lako lisitawi kokote duniani.

2. Uwaongoze Viongozi wote wa dini, wafanye kazi kwa amani ili kuleta maendeleo kwa watu.

3. Ulete amani katika familia zenye mafarakano, magomvi na chuki.

4. Uwape Wananchi moyo wa ushirikiano na amani ili kusitawisha ujirani mwema na kufanya kazi kwa pamoja na kuleta maendeleo katika vijiji vyao.

5. Wachungaji wa Betlehemu walimheshimu Mtoto Yesu kwa zawadi: Utuongoze sisi pia tumheshimu na kumwabudu kwa sala na kuwasaidia wenye shida.

6. Uyasaidie Mataifa na watu waliogombana, kupatana ili kusitawisha amani na mafanikio ya maisha.

Ee Mungu, Baba wa milele, Mwanao alizaliwa usiku Betlehemu katika ukimya. Tunakuomba kwa unyenyekevu wa Mwanao aliyezaliwa safarini, utufundishe kuridhika na hali yetu. Kwa njia ya Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba vipaji vyetu viyafae mafumbo ya kuzaliwa kwa Bwana tunayoyaadhimisha leo. Na kama vile huyu aliyezaliwa mtu leo aling'aa kuwa ni Mungu pia, hali kadhalika vipaji vyetu hivyo vya kidunia vituletee uzima wa kimungu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI wa Kuzaliwa kwa Bwana, I, II au III.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zek.9:9
Furahi sana, ee binti Sayuni; piga kelele, ee binti Yerusalemu; tazama, Mfalme wako anakuja; ni mtakatifu na mwokozi wa dunia.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sisi tunaoadhimisha kwa ibada yenye furaha kuzaliwa kwake Mwanao, utujalie tutambue kwa imani timilifu kina cha fumbo hili, na kulipenda kwa ari timilifu ya mapendo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.