KUZALIWA BWANA
25 DESEMBA
MASOMO MISA YA MCHANA
chagua MASOMO MISA YA ALFAJIRI
ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.9:6
Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani
mwake; naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu.
Utukufu husemwa
KOLEKTA:
Ee Mungu, ulimwumba mwanadamu katika hadhi ya ajabu, tena ukamtengeneza kwa namna ya
ajabu zaidi. Tunakuomba utujalie tuweze kushiriki umungu wake yeye aliyekubali kushiriki
ubinadamu wetu. Anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele
na milele.
SOMO 1: Isa.52:7-10
Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye
habari njema ya mambo mema Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki!
Sauti ya walinzi wako! Wanapaza sauti zao, wanaimba pamoja; Maana wataona jicho kwa jicho,
Jinsi Bwana arejeavyo Sayuni. Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, Enyi mahali pa Yerusalemu
palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, Ameukomboa Yerusalemu. Bwana ameweka wazi mkono
wake mtakatifu Machoni pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-6(K)3
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Miisho yote ya dunia imeuona
wokovu wa Mungu wetu.
2. Bwana ameufunua wokovu wake
Machoni pa mataifa amedhihirisha haki yake,
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
4. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.(K)
SOMO 2: Ebr.1:1-6
Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho
wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya
ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri
ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika
bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilorithi lilivyo tukufu kuliko lao. Kwa maana alimwambia malaika
yupi wakati wowote: Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye
atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika
wote wa Mungu.
SHANGILIO: Lk.2:10-11
Aleluya, aleluya!
Siku takatifu imetung'aria: enyi mataifa njoni mkamwabudu Bwana, kwa sababu leo mwanga mkubwa umeshuka
duniani.
Aleluya!
SOMO 3: INJILI: Yn.1:1-18
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu. Huyo
mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika
chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya
watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu ametumwa kutoka kwa
Mungu jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate
kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa hiyo nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako
nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa
yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake
hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale
waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa
mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona
utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Yohane alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya
kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika
utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa
Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati
wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
Nasadiki husemwa. Wote hupiga magoti yasemwapo maneno Akapata
mwili ...akawa mwanadamu.
MAOMBI
Ndugu wapendwa, Neno wa Mungu ni Mungu wa milele, hana mwanzo wala mwisho.
Lakini kwa enzi yake ametwaa mwili akawa na mwanzo kwa kuzaliwa mwanadamu. Tumshangilie Bwana wetu
Yesu kristo,
1. Ee Kristo, Mwanga wa Mungu: Utuangaze kuona, kutambua na kufuata mwanga wa kimungu.
2. Wewe ni Neno wa Mungu: Utuzibue masikio na kupokea neno lako ili lituangaze katika njia ya amri
za Mungu.
3. Wewe ni Njia ya Mungu: Uwasaidie viongozi wa Serikali wawaongoze watu kwa kutenda na kwa amani.
4. Wewe ni Utukufu wa Mungu: Utupe nguvu ya kuonja utukufu wako katika unyonge wetu.
5. Twakuomba udumishe amani katika familia zetu na Taifa letu.
Tuombe: Ee Mungu, Baba mtakatifu wa milele, Mwanao ndiye mpatanishi kati
yako na sisi wanadamu wakosefu. Twakuomba usikilize maombi yetu kwa njia ya huyo huyo Kristo Bwana
wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, ikupendeze sadaka ya sikukuu hii ya leo, iliyo fidia kamili ya upatanisho wetu,
na iliyowekwa kwetu kuwa utimilifu wa ibada ya kimungu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI wa Kuzaliwa kwa Bwana, I, II au III.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.98:3
Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu mwenye huruma, tunakuomba ili Mwokozi wa ulimwengu aliyezaliwa leo, kama vile
anavyotufanya kuwa watoto wa Mungu, atujalie pia uzima wa milele. Anayeishi na kutawala
milele na milele.