1

Daudi anahabarishwa juu ya kifo cha Sauli
1 Baada ya kifo cha Sauli, Daudi alirudi baada ya kuwashinda Waamaleki, akakaa Siklagi kwa muda wa siku mbili.
2 Siku iliyofuata, mtu mmoja kutoka kambi ya Sauli, mavazi yake yakiwa yamechanwa kwa huzuni na akiwa na mavumbi kichwani alimwendea Daudi. Alipomfikia Daudi, alijitupa chini mbele yake akamsujudia.
3 Daudi akamwambia, “Unatoka wapi?” Naye akamwambia, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.”
4 Daudi akamwambia, “Niambie mambo yalivyokuwa huko.” Yule mtu akamjibu, “Watu wetu wameyakimbia mapigano na wengi wetu wameuawa. Zaidi ya hayo, Sauli na mwanawe Yonathani pia wameuawa.”
5 Daudi akamwuliza yule kijana, “Unajuaje kuwa Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”
6 Yule kijana akamjibu, “Kwa bahati, nilikuwapo mlimani Gilboa. Nilimwona Sauli ameegemea mkuki wake na magari ya wapandafarasi ya adui zake yalikuwa yanamsonga sana.
7 Sauli alipotazama nyuma, aliniona, akaniita. Nilipoitika,
8 yeye aliniuliza mimi ni nani, nami nikamwambia kuwa mimi ni Mmaleki.
9 Hapo, akaniambia, ‘Karibia uniue maana nimejeruhiwa vibaya na maumivu ni makali. Lakini bado ningali hai’.
10 Hivyo, nilikwenda karibu naye na kumuua, kwa sababu nilikuwa na uhakika kuwa akianguka chini, hataweza kuishi zaidi. Lakini taji iliyokuwa kichwani pake na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, vyote nimekuletea wewe, bwana wangu.”
11 Daudi akayashika mavazi yake na kuyararua kwa huzuni. Hata watu waliokuwa pamoja na Daudi wakafanya vivyo hivyo.
12 Wakaomboleza, wakalia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Sauli, Yonathani mwanawe, na nchi ya Waisraeli, watu wa Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa wengi wao waliuawa vitani.
13 Daudi akamwuliza yule kijana aliyempasha habari, “Unatoka wapi?” Yeye akajibu, “Mimi ni Mmaleki, lakini ninaishi katika nchi yako kama mgeni.”
14 Daudi akamwuliza, “Ilikuwaje wewe hukuogopa kuunyosha mkono wako na kumuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta?”
15 Kisha, Daudi akamwita mmoja wa vijana wake akamwambia, “Muue mtu huyu!” Yule kijana alimpiga yule Mmaleki, naye akafa.
16 Daudi akasema, “Uwajibike wewe mwenyewe kwa kifo chako, maana umejishuhudia wewe mwenyewe kwa mdomo wako ukisema, ‘Nimemuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta.’”

Daudi aomboleza kifo cha Sauli na Yonathani
17 Daudi aliimba ombolezo lifuatalo kwa ajili ya Sauli na mwanawe Yonathani.
18 Daudi alisema watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hilo, nalo limeandikwa katika kitabu cha Yashari. Daudi aliimba,
19 “Walio fahari yako, ee Israeli, wameuawa milimani pako. Jinsi gani mashujaa walivyoanguka!
20 Jambo hilo msiuambie mji wa Gathi wala katika mitaa ya Ashkeloni. La sivyo, wanawake Wafilisti watashangilia, binti za wasiotahiriwa, watafurahi.
21 “Enyi milima ya Gilboa, msiwe na umande au mvua juu yenu. Wala mashamba yenu daima yasitoe chochote. Maana huko ngao za shujaa zilitiwa najisi, ngao ya Sauli haikupakwa mafuta.
22 “Upinde wa Yonathani kamwe haukurudi nyuma, upanga wa Sauli kamwe haukurudi bure, daima ziliua wengi. Naam, ziliua mashujaa.
23 “Sauli na Yonathani, watu wa ajabu na wakupendeza. Maishani na kifoni hawakutengana. Walikuwa wepesi kuliko tai, naam, wenye nguvu kuliko simba.
24 “Wanawake wa Israeli, mlilieni Sauli! Aliwavika mavazi mekundu ya fahari, aliyatarizi mavazi yenu kwa dhahabu.
25 “Jinsi gani mashujaa walivyoanguka! Wamekufa wakiwa katika mapambano. Yonathani analala, akiwa ameuawa milimani.
26 Nasikitika kwa ajili yako, ndugu yangu Yonathani. Umekuwa kwangu daima mtu wa kupendeza, pendo lako kwangu limekuwa la ajabu, la ajabu kuliko la mwanamke.
27 “Jinsi gani mashujaa wameanguka, na silaha zao zimeachwa, hazina kazi.”

Generic placeholder image