31

Kifo cha Sauli na wanawe
(Kumb 10:1-12)
1 Basi, Wafilisti walipigana vita dhidi ya Waisraeli; nao Waisraeli walikimbia mbele ya Wafilisti, na kuuawa katika mlima wa Gilboa.
2 Lakini Wafilisti wakamzingira Sauli na wanawe, kisha wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-shua, wana wa Sauli.
3 Vita vilikuwa vikali sana dhidi ya Sauli. Wapiga mishale walipomwona walimjeruhi vibaya.
4 Ndipo Sauli alipomwambia mtu aliyembebea silaha, “Chomoa upanga wako unichome nife, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanichoma upanga na kunidhihaki.” Lakini huyo aliyembebea silaha hakuthubutu kwa sababu aliogopa sana. Hivyo, Sauli alichukua upanga wake mwenyewe, na kuuangukia.
5 Halafu yule aliyembebea silaha alipoona kuwa Sauli amekufa, naye pia aliuangukia upanga wake, akafa pamoja na Sauli.
6 Hivyo ndivyo Sauli alivyokufa, na wanawe watatu, pia na mtu aliyembebea silaha pamoja na watu wake wote katika siku hiyohiyo moja.
7 Nao Waisraeli waliokuwa upande wa pili wa bonde, na wengine waliokuwa upande wa mashariki wa mto Yordani walipoona kuwa Waisraeli wamekimbia, naye Sauli na wanawe wamekufa, waliihama miji yao, wakakimbia. Wafilisti wakaenda na kukaa katika miji hiyo.
8 Kesho yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa walizikuta maiti za Sauli na wanawe mlimani Gilboa.
9 Walikata kichwa cha Sauli na kumvua silaha zake; halafu waliwatuma wajumbe katika nchi yao yote ya Filistia kutangaza habari njema nyumbani mwa sanamu zao na kwa watu.
10 Zile silaha zake waliziweka nyumbani mwa Maashtarothi; kisha wakautundika mwili wake kwenye ukuta wa mji wa Beth-sheani.
11 Lakini wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi waliposikia Wafilisti walivyomtendea Sauli,
12 mashujaa wote waliondoka, wakasafiri usiku kucha, wakaondoa mwili wa Sauli na miili ya wanawe kutoka ukuta wa Beth-sheani; wakaja nayo mpaka Yabeshi na kuiteketeza huko.
13 Baadaye, wakaichukua mifupa yao na kuizika chini ya mkwaju huko Yabeshi; nao wakafunga kwa muda wa siku saba.

Generic placeholder image