18

1 Sauli alipomaliza kuzungumza na Daudi, Yonathani mwana wa Sauli, alivutiwa sana na Daudi, akampenda kwa moyo wake wote kama alivyojipenda yeye mwenyewe.
2 Tangu siku hiyo, Sauli akamchukua Daudi nyumbani kwake, asimruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake.
3 Kwa kuwa Yonathani alimpenda Daudi kama roho yake, alifanya agano naye.
4 Alivua vazi alilovaa na kumpa Daudi pamoja na silaha zake, hata upanga, upinde na mkanda wake.
5 Kokote Daudi alikotumwa na Sauli, Daudi alifanikiwa. Hivyo, Sauli akamfanya kuwa mkuu wa jeshi lake. Jambo hilo liliwafurahisha watu wote hata watumishi wa Sauli.

Sauli anamwonea kijicho Daudi
6 Askari walipokuwa wanarudi nyumbani, pamoja na Daudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake kutoka kila mji katika Israeli walitoka kwenda kumlaki mfalme Sauli. Wanawake nao walikuwa wanaimba nyimbo za furaha, wakipiga matari na vinubi.
7 Pia walikuwa wanacheza na kuimba nyimbo za kuitikiana hivi: “Sauli ameua maelfu yake, na Daudi ameua makumi elfu yake.”
8 Sauli hakupendezwa na maneno ya wimbo huo, hivyo akakasirika sana. Akasema, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa maelfu tu. Lililobakia ni kumpa Daudi ufalme.”
9 Tangu siku hiyo, Sauli akawa anamwonea kijicho Daudi.
10 Kesho yake, roho mwovu kutoka kwa Mungu, alimvamia Sauli kwa ghafla, akawa anapayukapayuka kama mwendawazimu nyumbani kwake. Daudi alikuwa anapiga kinubi kama alivyofanya siku zote. Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake;
11 basi, alimtupia Daudi mkuki mara mbili kwani alifikiri, “Nitambana Daudi ukutani.” Lakini Daudi alikwepa mara zote mbili.
12 Sauli alikuwa anamwogopa Daudi kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye, lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwacha Sauli.
13 Hivyo, Sauli akamwondoa na kumfanya kiongozi wa wanajeshi 1,000. Naye Daudi akawaongoza vyema vitani.
14 Daudi alifanikiwa katika kila kitu alichofanya, kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye.
15 Sauli alipoona kufanikiwa kwa Daudi, akawa anamwogopa.
16 Lakini watu wote wa Israeli na Yuda walimpenda Daudi, kwani aliwaongoza vizuri vitani na kuwarudisha kwa mafanikio.

Daudi anamwoa binti wa Sauli
17 Sauli akamwambia Daudi, “Huyu ni Merabu, binti yangu mkubwa, nitakuoza awe mke wako kwa masharti mawili: Uwe askari wangu shupavu na mtiifu, upigane vita vya Mwenyezi-Mungu.” [Sauli alidhani kwa njia hiyo Wafilisti watamuua Daudi, ili kitendo hicho asikifanye yeye mwenyewe.]
18 Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani hata mfalme awe baba mkwe wangu? Ukoo wangu wenyewe na hata jamaa ya baba yangu si maarufu katika Israeli.”
19 Lakini, wakati ule ambapo Merabu binti yake Sauli angeozwa kwa Daudi, aliozwa kwa Adrieli kutoka mji wa Mehola.
20 Hata hivyo, Mikali binti mwingine wa Sauli alimpenda Daudi. Sauli alipoambiwa alifurahi sana.
21 Sauli alifikiri, “Ngoja nimwoze huyu ili awe mtego kwake. Na bila shaka Wafilisti watamuua.” Hivyo Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, “Sasa nitakuwa baba mkwe wako.”
22 Halafu Sauli aliwaamuru watumishi wake akisema “Ongea faraghani na Daudi na kumwambia, ‘Mfalme anapendezwa sana nawe, hata watumishi wake pia wote wanakupenda’. Hivyo, sasa kubali kuwa mkwewe mfalme.”
23 Basi, watumishi hao wa Sauli walimwambia Daudi maneno hayo faraghani, naye akawaambia, “Mimi ni mtu maskini na duni. Je mnadhani mfalme kuwa baba mkwe wangu ni jambo rahisi?”
24 Wale watumishi walimweleza Sauli kama Daudi alivyosema.
25 Sauli akawaambia, “Mwambieni Daudi hivi: ‘Kile ambacho mfalme anataka kama mahari ya binti yake ni magovi 100 ya Wafilisti, ili ajilipize kisasi cha adui zake.’” [Hivi ndivyo Sauli alivyopanga Daudi auawe na Wafilisti.]
26 Wale watumishi walipomweleza Daudi yale matakwa ya Sauli, Daudi alifurahi kuwa mfalme atakuwa baba mkwe wake. Kabla ya siku ya harusi,
27 Daudi na watu wake walikwenda, wakawaua Wafilisti 200 na kuyachukua magovi yao mpaka kwa mfalme Sauli. Hapo akamhesabia idadi kamili ili mfalme awe baba mkwe wake Daudi. Hivyo, Sauli akamwoza Daudi binti yake Mikali awe mke wake.
28 Lakini Sauli alipoona wazi kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Daudi, na kuwa Mikali binti yake alimpenda mno Daudi,
29 alizidi kumwogopa Daudi. Sauli akawa adui wa Daudi daima.
30 Jeshi la Wafilisti lilikwenda kupigana na Waisraeli, lakini kila mara walipopigana vita, Daudi alipata ushindi kuliko watumishi wa Sauli; hivyo jina lake Daudi likazidi kusifiwa sana.

Generic placeholder image