15

Vita dhidi ya Waamaleki
1 Samueli alimwambia Sauli, “Mwenyezi-Mungu alinituma kukupaka mafuta uwe mfalme wa watu wake wa Israeli. Sasa sikiliza maneno ya Mwenyezi-Mungu.
2 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa sababu waliwapiga Waisraeli walipokuwa wanatoka Misri.
3 Sasa, nenda ukawashambulie na kuangamiza vitu vyote walivyo navyo. Usiwaache hai, ila uwaue wote: Wanaume kwa wanawake, watoto wachanga na wanyonyao, ng'ombe, kondoo, ngamia na punda.’”
4 Sauli akaliita jeshi lake, akalikagua huko Telaimu. Kulikuwa na askari wa miguu 200,000 kutoka Israeli na 10,000 kutoka Yuda.
5 Halafu yeye na watu wake wakaenda kwenye mji wa Amaleki, wakawa wakivizia kwenye bonde.
6 Sauli akawaambia Wakeni, “Nendeni! Ondokeni! Tokeni miongoni mwa Waamaleki, la sivyo, nitawaangamiza pamoja nao. Ondokeni kwa sababu nyinyi mliwatendea wema Waisraeli walipotoka Misri.” Basi, Wakeni wakaondoka miongoni mwa Waamaleki.
7 Sauli aliwashinda Waamaleki kuanzia Havila hadi Shuri, mashariki ya Misri.
8 Alimteka mfalme Agagi wa Waamaleki akiwa hai. Akawaua watu kwa makali ya upanga.
9 Lakini Sauli na watu wake hawakumuua Agagi, wala kondoo bora kabisa, ng'ombe wazuri, ndama, wanakondoo na chochote kile kilichokuwa kizuri hawakukiangamiza. Lakini vitu vyote vibaya na visivyo na thamani waliviangamiza.
10 Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli,
11 “Ninajuta kwamba nimemfanya Sauli kuwa mfalme. Yeye ameacha kunifuata mimi na hajatimiza amri zangu.” Samueli alikasirika, akamlilia Mwenyezi-Mungu usiku kucha.
12 Samueli alisikia kuwa Sauli alikuwa amekuja huko Karmeli na amesimamisha mnara wa ukumbusho wake, na kwamba amekwenda Gilgali. Hivyo, kesho yake, Samueli aliamka asubuhi na mapema akaenda kukutana na Sauli.
13 Samueli alipomfikia Sauli, Sauli akamwambia Samueli, “Mwenyezi-Mungu na akubariki! Nimetekeleza amri ya Mwenyezi-Mungu.”
14 Samueli akamwambia, “Mbona nasikia mlio wa kondoo na ng'ombe?”
15 Sauli akajibu, “Watu waliwaacha hai kondoo na ng'ombe bora kabisa ili kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, lakini wengine wote tumewaangamiza.”
16 Samueli akamkatiza Sauli, “Nyamaza! Nitakuambia jambo aliloniambia Mwenyezi-Mungu leo usiku.” Sauli akasema, “Niambie.”
17 Samueli akamwambia, “Ingawa unajiona kuwa wewe si maarufu, je, wewe si kiongozi wa makabila ya Israeli? Mwenyezi-Mungu alikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.
18 Mwenyezi-Mungu alipokutuma alikuambia, ‘Nenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hadi umewaua wote!’
19 Kwa nini basi, hukuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu? Kwa nini mkakimbilia nyara na hivyo kutenda jambo ovu mbele ya Mwenyezi-Mungu?”
20 Sauli akajibu, “Nimetii sauti ya Mwenyezi-Mungu. Nilikwenda kule alikonituma Mwenyezi-Mungu; nimemleta Agagi mfalme wa Waamaleki, na nimewaangamiza kabisa Waamaleki.
21 Lakini watu walichukua nyara: Kondoo, ng'ombe na vitu vyote bora vilivyotolewa viangamizwe ili kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, huko Gilgali.”
22 Ndipo Samueli akamwambia, “Je, Mwenyezi-Mungu anapendelea zaidi dhabihu za kuteketezwa na matambiko, kuliko kuitii sauti yake? Tazama, kumtii yeye ni bora kuliko matambiko na kumsikiliza kuliko kumtambikia mafuta ya beberu.
23 Uasi ni sawa na dhambi ya kupiga ramli, na kiburi ni sawa na uovu na kuabudu vinyago. Kwa sababu umeikataa amri ya Mwenyezi-Mungu, naye amekukataa kuwa mfalme.”
24 Sauli akamwambia Samueli, “Nimetenda dhambi. Nimeasi amri ya Mwenyezi-Mungu na amri yako, kwa sababu niliwaogopa watu, nikawatii wao.
25 Lakini sasa nakuomba, unisamehe dhambi yangu. Niruhusu nirudi pamoja nawe ili niweze kumwabudu Mwenyezi-Mungu.”
26 Samueli akamjibu: “Kamwe, siwezi kurudi pamoja nawe. Wewe umeikataa amri ya Mwenyezi-Mungu, naye amekukataa kuwa mfalme juu ya Israeli.”
27 Samueli alipogeuka ili aende zake, Sauli akashika pindo la vazi lake, nalo likapasuka.
28 Ndipo Samueli alipomwambia Sauli, “Tangu leo Mwenyezi-Mungu ameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako na atampa mtu mwingine miongoni mwa jirani zako aliye bora kuliko wewe.
29 Na Mungu ambaye ni utukufu wa Israeli hadanganyi, wala habadili wazo lake. Yeye si binadamu hata abadili mawazo.”
30 Sauli akajibu, “Nimefanya dhambi. Hata hivyo, unistahi sasa mbele ya wazee wa watu wangu na Waisraeli. Niruhusu nirudi pamoja nawe ili nikamwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.”
31 Basi, Samueli akarudi pamoja naye mpaka Gilgali na Sauli akamwabudu Mwenyezi-Mungu.
32 Kisha Samueli akasema, “Nileteeni hapa Agagi mfalme wa Waamaleki.” Agagi akamwendea Samueli akiwa mwenye furaha kwani alifikiri, “Uchungu wa kifo umepita.”
33 Samueli akasema, “Kwa kuwa upanga wako umewafanya akina mama wengi wasiwe na watoto, ndivyo na mama yako atakavyokuwa bila mtoto miongoni mwa akina mama.” Akamkatakata Agagi vipandevipande mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Gilgali.
34 Kisha, Samueli akaenda Rama; na mfalme Sauli akarudi nyumbani kwake huko Gibea.
35 Tangu siku hiyo, Samueli hakumwona tena Sauli, mpaka siku alipofariki. Hata hivyo Samueli alimlilia Sauli. Naye Mwenyezi-Mungu alisikitika kwamba alikuwa amemtawaza Sauli mfalme juu ya Israeli.

Generic placeholder image