28

1 Baada ya muda fulani, Wafilisti walikusanya majeshi yao tayari kwenda kupigana na Waisraeli. Akishi akamwambia Daudi, “Uelewe vizuri kwamba wewe na watu wako mnapaswa kwenda pamoja nami kupigana vita.”
2 Daudi akamjibu Akishi, “Naam! Utaona kitu ambacho mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamwambia, “Nami nitakufanya kuwa mlinzi wangu binafsi wa maisha.”
3 Wakati huu, Samueli alikuwa amekwisha fariki, na Waisraeli wote walikuwa wamekwisha mwombolezea na kumzika katika mji wake Rama. Sauli alikuwa amewafukuza kutoka nchini watabiri na wachawi.
4 Wafilisti walikusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu; na Sauli aliwakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao kwenye mlima Gilboa.
5 Sauli alipoona jeshi la Wafilisti alianza kuogopa, akaanza kutetemeka kwa hofu aliyokuwa nayo moyoni mwake.
6 Hata alipomwomba Mwenyezi-Mungu shauri, Mwenyezi-Mungu hakumjibu kwa ndoto, kwa mawe ya kauli, wala kwa njia ya manabii.
7 Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke ambaye anaweza kutabiri ili nimwendee na kumtaka shauri.” Watumishi wake wakamjibu, “Yuko mtabiri mmoja huko Endori.”
8 Basi, Sauli akajigeuza na kuvaa mavazi mengine, akaenda huko pamoja na watu wake wawili. Walifika kwa huyo mwanamke usiku, akamwambia, “Nitabirie kwa pepo, umlete duniani yeyote nitakayekutajia.”
9 Yule mwanamke akamwambia, “Wewe unajua kwa hakika kuwa mfalme Sauli amewaangamiza kabisa watabiri na wachawi wote katika nchi ya Israeli. Sasa kwa nini unaniwekea mtego wa kuninasa na kuniua?”
10 Sauli akamwapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akisema, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba hakuna adhabu yoyote itakayokupata kutokana na jambo hili.”
11 Yule mwanamke akamwuliza, “Je, nikuletee nani kutoka huko?” Sauli akajibu, “Niletee Samueli.”
12 Yule mwanamke alipomwona Samueli alilia kwa sauti kuu, akamwambia Sauli, “Kwa nini umenidanganya? Wewe ni Sauli!”
13 Mfalme Sauli akamwambia, “Usiogope! Unaona nini?” Yule mwanamke akamjibu, “Naona mungu akitokea ardhini.”
14 Sauli akamwambia mwanamke, “Ni mfano wa nani?” Yule mwanamke akamwambia, “Mwanamume mzee anapanda juu, naye amejizungushia joho.” Hapo, Sauli akatambua kwamba huyo ni Samueli. Sauli akainama hadi chini, na kusujudu.
15 Samueli akamwambia Sauli, “Kwa nini unanisumbua kwa kunileta juu?” Sauli akamjibu, “Mimi nina taabu kubwa! Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, na Mungu amenipa kisogo; hanijibu tena kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Ndio maana nimekuita unijulishe la kufanya.”
16 Samueli akasema, “Kwa nini unaniomba shauri ambapo Mwenyezi-Mungu amekupa kisogo na amekuwa adui yako?
17 Mwenyezi-Mungu amekutendea kile alichokuambia kwa njia yangu. Mwenyezi-Mungu ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, na amempa Daudi jirani yako.
18 Maana, wewe hukuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, wala hukuitekeleza ghadhabu yake dhidi ya Waamaleki. Ndio maana leo Mwenyezi-Mungu amekutendea mambo haya.
19 Zaidi ya hayo, Mwenyezi-Mungu atakutia wewe pamoja na Waisraeli wote mikononi mwa Wafilisti. Kesho, wewe na wanao mtakuwa pamoja nami; hata jeshi la Israeli Mwenyezi-Mungu atalitia mikononi mwa Wafilisti.”
20 Ghafla, Sauli akiwa na hofu kutokana na maneno ya Samueli, alianguka kifudifudi; hakuwa na nguvu zozote; kwa kuwa alikuwa hajala chochote kwa siku nzima, usiku na mchana.
21 Ndipo yule mwanamke alipomwendea Sauli, na alipoona kuwa Sauli ameshikwa na hofu mno, alimwambia, “Mimi mtumishi wako nimehatarisha maisha yangu kwa kufanya kile ulichoniambia nikufanyie.
22 Sasa, nisikilize mimi mtumishi wako; nitakuandalia mkate ili ule nawe utakuwa na nguvu za kuendelea na safari yako.”
23 Lakini Sauli alikataa na kusema, “Sitakula.” Lakini watumishi pamoja na yule mwanamke, walimsihi ale, naye akawasikiliza. Hivyo aliinuka kutoka chini na kukaa kwenye kitanda.
24 Yule mwanamke alikuwa na ndama wake mmoja nyumbani aliyenona, akamchinja haraka, akachukua unga wa ngano, akaukanda, akatengeneza mkate usiotiwa chachu.
25 Akampa Sauli, akawapa pia watumishi wake, nao wakala. Halafu wakaondoka na kwenda zao wakati huohuo usiku.

Generic placeholder image