11

Upendo wa Mungu wapita hasira yake
1 “Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda, Kutoka Misri nilimwita mwanangu.
2 Lakini kadiri nilivyozidi kuwaita, ndivyo walivyozidi kwenda mbali nami; waliendelea kuyatambikia Mabaali, na kuvifukizia ubani vinyago vya miungu.
3 Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea! Mimi mwenyewe niliwachukua mikononi mwangu; lakini hawakutambua kuwa mimi ndiye niliyewatunza.
4 Niliwaongoza kwa kamba za huruma naam, kwa kamba za upendo; kama baba amwinuaye mtoto mpaka shavuni mwake, ndivyo nami nilivyokuwa kwao. Mimi niliinama chini na kuwalisha.
5 Basi, watarudi nchini Misri; watatawaliwa na mfalme wa Ashuru, kwa sababu wamekataa kunirudia.
6 “Upanga utavuma katika miji yao, utavunjavunja miimo ya malango yake na kuwaangamiza katika ngome zao.
7 Watu wangu wamepania kuniacha mimi, wakiitwa waje juu, hakuna hata mmoja anayeweza.
8 Ewe Efraimu, nawezaje kukuacha? Nawezaje kukutupa ewe Israeli? Nitawezaje kukufanya kama mji wa Adma? Nitawezaje kukutenda kama Seboimu! Nazuiwa na moyo wangu; huruma yangu imezidi kuwa motomoto.
9 Nitaizuia hasira yangu kali; sitamwangamiza tena Efraimu, maana mimi ni Mungu, wala si binadamu. “Mimi ndimi Mtakatifu miongoni mwenu, nami sitakuja kuwaangamiza.
10 “Watanifuata mimi Mwenyezi-Mungu ningurumaye kama simba; nitakaponguruma watanijia toka magharibi wakitetemeka.
11 Watakuja kutoka Misri wakitetemeka kama ndege, wataruka kutoka Ashuru kama hua nami nitawarudisha makwao; mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
12 Watu wa Efraimu wananirundikia uongo, na Waisraeli udanganyifu. Watu wa Yuda, wananiasi mimi Mungu Mtakatifu.

Generic placeholder image